*APR yanawiri Morogoro
Na Zahoro Mlanzi
MAMBO bado magumu kwa wenyeji wa mashindano ya Kagame Castle Cup baada ya Yanga kulazimishwa sare ya mabao 2-2 na El-Mereikh ya
Sudan katika mchezo uliopigwa jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ikiwa ni siku moja tangu wawakilishi wengine wa Tanzania Simba kulazimishwa suluhu na Vital'O ya Burundi.
Katika mechi hiyo maelfu ya mashabiki wa Yanga, walijitokeza kwenda kuwaona wachezaji wapya waliosajiliwa na timu hiyo wakiwa na nyuso za furaha, lakini baada ya dakika 90 kumalizika hali haikuwa hivyo.
Kabla ya mchezo huo wa jana kuanza, Maofisa wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), wakiongozwa na Katibu Mkuu wao, Nicholaus Musonye na Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura walihaha kushughulikia suala la Godfrey Bonny wa Yanga kuwepo katika orodha ya wachezaji wa akiba.
Suala hilo lilionekana tata, baada ya kubainika kwamba Bonny hakuwepo katika orodha ya wachezaji 20 waliotangazwa na Yanga kwa ajili ya mashindano hayo, lakini baadaye iliamuliwa aondolewe na kukaa jukwaani.
Katika mchezo huo, timu zote zilianza kwa kasi lakini El Mereikh ilifanya shambulizi la kushtukiza dakika ya pili na kufunga bao lililofungwa na Kelechi Osunwa kwa kichwa akiunganisha krosi ya Karim Eddafi.
Baada ya kufungwa kwa bao hilo, Yanga ilitulia na katika hali isiyotarajiwa na mashabiki waliokuwepo uwanjani hapo dakika ya tano kiungo Ahmed Albasha, alimrudishia mpira kipa wake, Isam Elhadari kwa shuti lililomzidi mbio na kutinga wavuni.
Timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu huku El-Mereikh, ikionekana kutandaza kandanda safi kutokana na pasi zao walizopiga kumfikia mlengwa.
Dakika ya 11, Jerson Tegete wa Yanga nusura aifungie timu yake bao la pili baada ya kupiga shuti nje ya eneo la hatari lililopanguliwa na Elhadari na mabeki kuondosha hatari.
Yanga ilipata pigo baada ya Tegete kuumia nyama za miguu na nafasi yake kuchukuliwa na Keneth Asamoah, ambaye dakika ya 35 alimpa presha beki Saeed Mustapha na kujikuta akikwamisha mpira wavuni katika harakati za kuokoa krosi iliyopigwa na Oscar Joshua.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na El-Mereikh katika dakika 10 za kwanza walionekana kuridhika na matokeo lakini dakika ya 63 ilifanya shambulizi la kushtukiza na kuzaa matunda kwa bao la kusawazisha lililofungwa na Jonas Sakuwaha kwa shuti lililogonga mtambaa wa panya na kujaa wavuni.
Timu hizo ziliendelea kuoneshana kazi kwa kushambuliana kwa zamu ambapo dakika ya 84, Rashidy Gumbo nusura aifungie Yanga bao la ushindi baada ya kupiga shuti lililotoka sentimeta chache pembeni ya goli kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na Julius Mrope.
Mbali na matokeo hayo, katika mchezo huo kivutio kikubwa kilikuwa ni Mrope kwa upande wa Yanga, ambaye alionekana kuwasumbua mabeki wa El-Mereikh na Eddafi kwa upande wa wageni hao ambaye alikuwa akiwachachafya mabeki Godfrey Taita na Chacha Marwa wa Yanga.
Yanga: Yaw Berko, Taita, Joshua, Nadir Haroub 'Canavaro', Marwa, Nurdin Bakari, Mrope, Gumbo, Davies Mwape, Tegete/Asamoah na Kigi Makasi.
Wakati huohuo, kutoka Morogoro mabingwa watetezi, timu ya APR ya Rwanda imeibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Port ya Djibouti katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Jamhuri mkoani humo.
Timu zetu zimezoea kucheza mpira wa mdomoni pamoja na kwenye magazeti wakati wenzao huwa wanacheza mpira wa vitendo.
ReplyDelete