Na Zahoro Mlanzi
BARAZA la Vyama vya Mpira wa Miguu Kusini mwa Afrika (COSAFA), limeipanga timu ya taifa ya wanawake 'Twiga Stars' Kundi A lenye timu za Lesotho, Botswana
na wenyeji Zimbabwe.
Twiga Stars itashiriki mashindano hayo ya wanawake ikiwa timu mwalikwa pamoja na Msumbiji, itaanza kampeni yake ya kutwaa ubingwa Julai 2 mwaka huu kwa kuumana na Botswana.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema Twiga Stars itacheza siku hiyo ya ufunguzi kwenye Uwanja wa Gwanzura nchini humo ambapo mashindano hayo yatafikia tamati Julai 9.
Alisema siku itakayofuata itacheza na Lesotho kwenye Uwanja wa Rufaro na kumalizia mechi ya mwisho ya kundi hilo Julai 5 mwaka huu kwa kuumana na wenyeji Zimbabwe, kwenye Uwanja wa Gwanzura.
"Timu nyingine zitakazoshiriki michuano hiyo ambayo mechi zake pia zitapigwa katika viwanja hivyo ni Afrika Kusini, Zambia, Msumbiji na Malawi na kwamba kila kundi litatoa timu mbili kuingia nusu fainali," alisema Wambura.
Alisema mashindano hayo yataisaidia timu hiyo kujiandaa na michuano ya michezo ya Afrika itakayofanyikia Maputo, Msumbiji Septemba mwaka huu.
Wambura alisema timu hiyo iliingia kambini tangu wiki iliyopita ikiwa na kikosi cha wachezaji 25 kikiwa chini ya makocha, Charles Mkwassa akisaidia na Nasra Mohamed.
No comments:
Post a Comment