13 June 2011

Wawili wavuliwa uongozi CHADEMA

Na Suleiman Abeid, Meatu

KATIKA kile kinachoashiria ni kupiga vita vitendo vya ufisadi, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wilayani Meatu mkoani Shinyanga kimewatimua viongozi wake
wawili wanaotuhumiwa kufanya ubadhirifu wa sh. milioni 4.5.

Viongozi waliovuliwa uongozi ni pamoja na Katibu wa Wilaya, Bw. Godlizen Malegeza na mwenzake ambaye hakupatikana kujibu tuhuma dhidi yake, ambao kwa pamoja wanatuhumiwa kufuja kiasi cha shilingi milioni 4.5 za chama hicho na kuzitumia katika matumizi binafsi na wameagizwa kuzirejesha.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa juzi katika mkutano mkuu wa chama hicho
uliofanyika mjini Mwanhuzi kiasi hicho cha fedha kilitolewa na Mbunge wa Jimbo la Meatu, Bw. Meshack Opulukwa (CHADEMA) ili kusaidia kuanzisha mradi utakaokisaidia chama hicho kujipatia fedha badala ya kutegemea misaada kutoka makao makuu.

Pia viongozi hao wanatuhumiwa kukiuka katiba na kanuni za chama hicho ikiwemo suala la kulinda maadili na nidhamu kwa mujibu wa ibara ya 10.1 ya katiba ya CHADEMA kutokana kitendo chao cha kumdhalilisha mbunge wakidai aliokotwa mitaani.

Uamuzi wa kuwavua uongozi viongozi hao ulitangazwa rasmi juzi na mwenyekiti wa muda wa CHADEMA, Bw. Peter Mkiru katika mkutano mkuu maalumu ulioitishwa ili kujadili malalamiko ya wanachama waliokuwa wakidai kuwepo kwa ubadhirifu wa fedha ndani ya chama hicho.

Ilielezwa katika mkutano huo maalumu kuwa viongozi hao walitumia fedha hizo kwa kufanya biashara ya kusafirisha mbuzi kutoka nchini kwenda kuwauza Kenya kwa kisingizio mapato yake yangeingizwa katika mfuko wa chama, lakini faida iliyopatikana kutokana na biashara hiyo haikuweza kuonekana.

Kukwama kwa mradi huo wa kusafirisha mbuzi kulisababisha malalamiko mengi kutoka kwa wanachama ambao waliomba kuitishwa kwa mkutano mkuu ili wapewe taarifa rasmi huku wakidai kuwa suala la ufisadi halipaswi kupewa nafasi ndani ya CHADEMA.

Hata hivyo tayari viongozi hao wameisha rejesha sh. milioni 2.3 na hivi sasa bado wanadaiwa sh. milioni 1.6 ambazo wametakiwa kuhakikisha wanakamilisha kulipa deni hilo vinginevyo watachukuliwa hatua za kisheria.

Akijibu tuhuma hizo, Bw. Malegeza pamoja na kukiri kuwapo suala la fedha, alisema kikao kilichochukua maamuzi dhidi yao hakikuwa si halali, hivyo yeye na mwenzake wameshawasilisha malalamiko kwa uongozi wa mkoa na taifa kupinga.

2 comments:

  1. CHADEMA HONGERENI KWA KUONYESHA MFANO KWA CCM,WEZI WANAFUKUZWA CHAMANI HAWAFANYIWI VIKAO VYA CHUMBANI NA KUPEWA SIKU 90 KUJIFIKIRIA KAMA WATOKE AU LA, WEZI WAKITHIBITIKA WANAFUKUZWA NA SIYO KUBEMBELEZWA KUOMBWA WAJIFIKIRIE NA KUJIHUKUMU WENYEWE DAWA YAO NI KUWA KICKED OUT.

    ReplyDelete
  2. danganya toto bado wamo uliza tunaoishi meatu

    ReplyDelete