Na Jumbe Ismailly, Singida
WALIMU wastaafu waliofanya kazi kwa mikataba katika shule za sekondari kwenye Manispaa ya Singida wanaidai serikali sh. 45,759,336.80 zikiwa ni mishahara
yao pamoja na makato holela waliyokuwa wakikatwa wakati wa utumishi wao huo.
Katika barua ya wazi ya wastaafu hao kwenda kwa Waziri Mkuu ambayo himesainiwa kwa niaba ya wastaafu hao, Bw. Lazaaus Ntandu imeeleza kuwa madai hayo ni katika kipindi cha kuanzia Novemba Mosi, 2007 hadi Jan 30, 2009.
Kwa mujibu wa maelezo ya barua hiyo kiasi hicho cha fedha ni kwa ajili ya walimu wastaafu wanne tu waliokuwa wakifundisha kwenye baadhi ya shule za sekondari na kwamba kila mmoja anaidai serikali sh. 11,439,844.20 katika kipindi hicho.
“Sisi walimu tulijiorodhesha hapa chini tuliajiriwa na serikali Novemba Mosi, 2007 ili tufundishe katika shule za sekondari za Manispaa ya Singida ,na aliyetuajiri ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, ambaye mpaka sasa yuko kimya na
madai yetu,”ilisema sehemu ya barua hiyo yenye kurasa mbili.
“Kabla ya kufafanua madai yetu,sisi wazee na walimu wastaafu tunampongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kukemea uzembe na utendaji mbaya wa wizara mbalimbali katika hotuba yake ya ufunguzi wa semina elekezi ya mawaziri iliyofanyika mjini Dodoma Mei 5, mwaka huu,” walisisitiza wazee hao.
Walifafanua wastaafu hao kwamba hawamshangai Mbunge wa Kigoma mjini kwa tiketi ya CHADEMA, Bw. Zito Kabwe anapokuwa akisema kuwa serikali imefilisika, bali wanamshangaa Waziri wa Fedha, Bw. Mustafa Mkulo anapopinga kauli hiyo wakati ameshindwa kuwalipa madai yao hayo.
Hata hivyo barua hiyo iliwataja walimu wastaafu hao wanadai kiasi hicho cha fedha huku check namba na namba za mafaili yao zikiwa kwenye mabano kuwa ni pamoja na Lazaaus N. Ntandu (C/No.11361332 na ED/PF 9310), Maulidi H. Bura (C/NO.11361354 na ED/PF1501), Jacob M.Mande (C/NO.11361321 na ED/PF1498) na Manase Y.Mbogo
(C/NO.11361343 na ED/PF 1499).
Waliweka wazi madai yao katika vipengere mbalimbali kuwa ni pamoja na mishahara yao ya miezi 15 kuanzia Novemba Mosi, 2007 hadi Januari 30, 2009, makato ya PSPF kuanzia Februari 2007
hadi Oktoba 2009, makato ya Bima ya Afya kuanzia Februari 2007 hadi Okt 2009 walipoanza kulipwa mishahara yao na asilimai 25 ya kiinua mgongo ya mishahara ya kipindi cha miezi 24 kama ilivyotamkwa katika mikataba yao kwenye aya ya 16(1).
No comments:
Post a Comment