08 June 2011

Hatimaye Mbunge Sakaya aachiwa huru

Humphrey Shao na Salim Nyomolelo

MBUNGE wa Viti Maalumu, Bi. Magdalena Sakaya na wenzake wameachiwa huru baada ya mahakama kubadili masharti ya dhamana yaliyokuwa yamewashinda na
kuendelea kusota rumande.

Hatua hiyo imechukuliwa na Mahakama ya Wilaya ya Urambo baada ya Wakili wa Chama cha Wananchi (CUF), Bw. Twaha Taslima kuwasilisha ombi la kutaka kesi hiyo itajwe kabla ya muda uliopangwa, na kuomba masharti yanadilishwe.

Mbali na Bi. Sakaya, wengine wanaoshtakiwa ni Bw. Yasin Mrotwa, Bw. Doyo Hassan na Bi. Zainabu Nyumba na wajumbe wa Baraza Kuu, Bw. Hashimu Bakari, Bw. Amir Kirungi na viongozi wengine waandamizi saba wa chama hicho.

Wakati hayo yakiendelea CUF jana iliitisha mkutano na waandishi wa habari na kumtaka Spika wa Bunge, Bi. Anna Makinda kuacha tabia ya kuegemea upande mmoja wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) na kuwajibika kwa wabunge wote walioko ndani ya bunge lake.

Mwenyekiti wa Chama hicho, Prof. Ibrahim Lipumba alitumia mkutano huo kulaani kitendo alichoita ukiukwaji wa haki za binadamu, kilichofanywa na Mahakama ya Wilaya Urambo.

"Inatia aibu, spika ni kiongozi wa wabunge wote nchini Tanzania sio CCM tu, hivyo ilimpasa kuchukua hatua ya kuwatetea wabunge wake pindi wanaponyanyaswa na sheria za nchi kukiukwa kwa ajili ya maslahi ya watu binafsi," alisema Prof Lipumba. 

Alisema kuwa chama chake kimewasilisha ombi kwa taasisi ya haki za binadamu kutaka kitendo hicho kichunguzwe ili haki itendeke.

Alisema kuwa katika hali ya kushangaza kiongozi wa kwanza kupandishwa kizimbani alikuwa ni Idd Matola katika kesi ya jinai Namba 60 /2011 ambapo dhamana yake iliwekwa wazi na wadhamini walisimama kuanza taratibu, na hakimu Bulugu alimtaka mwendesha mashtaka athibitishe hati za dhamana na baada ya kufanya hivyo, hakimu aliweka pingamizi.

Alisema kuwa ilipotajwa kesi ya jinai namba 57/2011, mwendesha mashtaka alisema hana pingamizi na dhamana kwa kuwa hali ya kata na sehemu vurugu ilipotokea pako shwari. Katika vurugu hizo, mbunge huyo anadaiwa kufanya mkutano bila kibali na polisi walipokwenda kuuvunja vurugu zikatokea na mtoto mmoja kuuawa  na wengine wawili kujerihiwa miguuni kwa risasi.

"Hata hivyo, hakimu huyo alitoa masharti magumu ambayo Wakili wa Washtakiwa, Bw. Twaha Taslima anaendelea kuomba mahakama iyatazame upya kwa kuwa kupata hati ya nyumba katika eneo hilo ni kazi ngumu kwa kuwa nyingi hazijasajiliwa.

Baada ya watuhumiwa hao kuachiwa huru baada ya kupokea barua za wadhamini, kesi hiyo iliahirshwa hadi Julai 11, mwaka huu.

2 comments:

  1. Sakaya hamia chadema, Mwenyekiti wako, Katibu na Mweka hazina wamekutosa; lakini unatosha kwa vita ya ustawi wa nchi hii, na ukiwa chadema utafanya mambo makubwa

    ReplyDelete
  2. ATFANYA NINI WENYEWE WAMESHINDWA ATAWEZA YEYE?NYIE MNA MAJUNGU HUYU NI CUF DAMU NA HAWEZI KUHAMIA CHAMA CHA WABABAISHAJI WAROHO WA MADARAKA HAMNA TOFAUTI NA MASHEMEJI ZENU CCM.POLE MAMA UMEONYESHA UKOMAVU KISIASA.ACHANA NA WAROPOKAJI KAMA WANAKUNYWA MAJI YA CHOONI.

    ReplyDelete