24 June 2011

Waghana kuzinoa Simba, Yanga

*Ni Asante Kotoko na Hearts of Oak

Na Mwandishi Wetu

TIMU za Asante Kotoko na Hearts of Oak za Ghana, zinatarajiwa kuzinoa makali Simba na Yanga Julai 16 na 17, mwaka huu katika mashindano ya
Kimataifa yatakayoshirikisha timu nne kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Lumuli Marketing, Sidwell Jan alisema mashindano hayo imeandaliwa kwa ushirikiano wa kampuni hiyo na Octagon kwa lengo la kuonesha viwango vyao katika soka na kuwaongezea uzoefu katika mashindano ya kimataifa.

Alisema klabu zote zimethibitisha kushiriki mashindano hayo ya timu nne na kwamba washindi watajipatia makombe, medali na heshima na kwamba Watanzania watarajie kupata burudani ya aina yake.

"Michuano hiyo itakuwa ikifanyika kila mwaka na watakuwa wakizialika timu zenye historia kubwa kwenye mchezo huo Afrika, kwani kwa kufanya hivyo klabu za Tanzania zitanufaika na michezo hiyo," alisema Jan.

Naye Mkurugenzi wa Octagon, Bonga Sebesho alisema timu za Tanzania zitapata uzoefu mkubwa kwa kucheza na timu zenye viwango vya juu Afrika na pia makocha wa timu hizo watapata fursa ya kubadilishana uzoefu na wenzao.

Alisema wakati michezo hiyo ikiendelea kutakuwa na burudani mbalimbali za muziki na promosheni, ambapo mashabiki watajishindia zawadi zitakazotolewa na kampuni hizo.

ASebosho alisema mapato yatakayopatikana kwa baadhi ya mechi yatapelekwa kwa shule za msingi, ambazo zimechaguliwa na kwamba shule hizo zitapata kompyuta pamoja na vifaa vya michezo.

Aliongeza kwamba, mechi hizo zitarushwa na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) ambapo pia ni mshirika katika michezo hiyo na kwamba siku za usoni, wataonesha zawadi na medali zitakazoshindaniwa.

No comments:

Post a Comment