KAMPALA,Uganda
MADAKTARI nchini Uganda, wanajiandaa kuwafanyia upasuaji mapacha waliozaliwa hivi karibuni katika eneo la Kabale wakiwa wameungana sehemu ya
kifuani.
Habari kutoka nchini humo zilieleza jana kuwa upasuaji huo utafanyika hivi karibuni katika hospitali ya Mulago na kazi hiyo itawashirikisha wataalamu 10 wa afya.
“Wataalamu hao ni pamoja na naibu Mkurugenzi Mtendaji, Doreen Male,” alisema msemaji wa hospitali hiyo, Bw. Dan Kimosho.
Alisema kuwa hivi sasa madaktari wanangojea watoto hao ambao tayari wapo kwenye hospitali hiyo ya Mulago wafikishe uzito wa kilo 10 kabla ya upasuaji huo kufanyika.
Watoto hao ambao wote ni wa kiume walizaliwa na mwanamke mwenye umri wa miaka 24, Bi.Rosette Tusiime mkazi wa eneo la Kekubo lililopo katika Manispaa ya Kabale wakiwa wameungana sehemu ya kifuani.
Bw. Kimosho alisema kuwa uchunguzi unaonesha kuwa baadhi ya viungo vya mwili vimekaribiana sana lakini akasema kuwa viungo hivyo vipo tofauti.
Alifafanua kuwa mapacha hayo hawachangii ini moja kama taarifa za awali zilivyokuwa zikieleza, lakini hata hivyo Bw. Kimosho,alisema kuwa upasuaji huo utakuwa ni wa gharama.
“Nawaomba wanaonitakia mema maisha ya watoto hawa kutoa msaada wa kifedha ili kuhakikisha maisha yao yananusurika,”alisema.
Kwa upande wake Bi. Tusiime alisema kuwa watoto hao wananyonya vizuri na hali zao ni njema.
Hii itakuwa ni mara ya kwanza kufanyika upasuaji kama huo nchini Uganda.
Wataalam wa afya wanaeleza kwamba kesi ya kuzaliwa mapacha walioungana ni matokeo ya kushindwa kutenganishwa kiini tete.
Kwa mujibu wa watalam hao, mapacha wa aina hiyo ufanana hata chembechembe za vinasaba kutokana na kuzaliwa wakiwa na jinsia moja baada ya kutoka ndani yai moja hivyo kushirikiana katika ukuaji na hata kondo la nyuma.
Wataalam hao wanadai kuwa hatua za ukuaji wa yai hilo uanza kugawanyika na kufahamika kuwa ni la watoto mapacha katika wiki chache baada ya mimba kutunga, lakini baadaye ukuaji huo ukasimama kabla ya mchakato kukamilika.(New Vision).
No comments:
Post a Comment