24 June 2011

Michuano ya gofu kutimua vumbi leo

Na Amina Athumani

WACHEZA Gofu 100 kutoka mikoa mbalimbali nchini, wanatarajia kuchuana kesho katika mashindano ya gofu ya '1 & M Bank Golf Tournement', yatakayofanyika katika viwanja
vya Gymkhana Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya Gymkhana juzi, nahodha wa klabu hiyo Joseph Tango, alisema mashindano hayo yameandaliwa na Gymkhana na kudhaminiwa na benki ya I & M kwa lengo la kukuza na kuendeleza mchezo huo ikiwa pia ni moja ya maandalizi ya mashindano ya ndani na nje ya nchi.

"Kwa sasa tunakabiliwa na mashindano mbalimbali yakiwemo ya Olimpiki, hivyo mashindano haya ni sehemu ya maandalizi ya kuiandaa timu yetu ya Tanzania ambapo pia yataendelea kuimarisha vipaji vya wanamichezo wetu hapa nchini," alisema Tango.

Alisema mashindano hayo yatawajenga vizuri wachezaji wa klabu hiyo, katika kufanya vyema kwenye michuano ya taifa yatakayofanyika Jijini Arusha mwanzoni mwa Julai, pamoja na mashindano ya Olimpiki yatakayofanyika Scotland.

Tango amewashukuru wadhamini hao kwa kujitolea kudhamini mashindano hayo, kwa kuwa yataboresha vipaji vya wachezaji wa Tanzania.

Mashindano hayo yatatumia zaidi ya sh. milioni 10 kutoka kwa wadhamini hao, ambazo zimegawanywa katika zawadi na vifaa mbalimbali vya mchezo huo.

No comments:

Post a Comment