28 June 2011

Viongozi TLP wazidi kumkaba koo Mrema

Na Agnes Mwaijega

VIONGOZI wa Chama cha Tanzania Labour (TLP) wamemtaka Mwenyekiti wa chama hicho ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Vunjo, Bw. Augustino Mrema kujiuzulu kwa
madai kwamba ameshindwa kukiendesha chama hicho.

Pia wamelaani na kukanusha kauli iliyotolewa na Bw. Mrema wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma wiki iliyopita kwamba viongozi hao ni mizigo, wahuni na hawana chochote wanachokifanya kwa ajili ya maendeleo ya chama.

Wakati viongozi hao wakiendelea na mkutano wa waandishi wa habari kueleza hayo katika Ukumbi wa Idara ya Habari (Maelezo), walijitokeza baadhi ya watu wakavamia mkutano huo wakisambaza taarifa ya kukanusha madai hayo, na baadaye kuishia mikononi mwa pilisi.

Watu hao waliodai ni wanachama wa TLP walivamia na kuanza kugawa taarifa kwa waandishi wa habari ambayo haikuwa inaendana na kile anachokizungumza Bw. Tao, hivyo kusababisha mkanganyiko ndani ya ukumbi.

Waaandishi wa habari walipomuhoji Bw. Tao kwamba kwa nini taarifa waliyopewa haiendani na anachokizungumza, alidai kwamba haijui taarifa hiyo wala walioisambaza.

Alisema taarifa ya kile anachokizungumza anayo na haina uhusiano na iliyosambazwa na watu waliodaiwa kuvamia mkutano wake na waandishi wa habari.

Taarifa hiyo iliyosambazwa kinyemela, ilikuwa na lengo la kukanusha habari zilizochapishwa juzi kwenye vyombo vya habari kuwa Mrema sasa kufukuzwa kwenye nyumba anayoishi, ilikuwa imesainiwa na Bw. Tao, ambaye hata hivyo alikana kuitambua.

Kwa upande wake Bw Andason Temu ambaye ndiye aligawa taarifa hiyo alidai kuwa Bw. Tao ndiye aliyemwambia aje nayo Maelezo kwa ajili ya kuwapa waandishi wa habari.

Kutokana na mkanganyiko huo, Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) walifika na kuwachukua waliodaiwa kuvamia mkutano na kuwapeleka kituoni.

Kabla ya tafrani hiyo, viongozi hao walipinga kauli ya Bw. Mrema kwamba TLP haina viongozi mikoani na kubainisha kuwa wamechoshwa na vitendo vya kiongozi huyo, na kwamba kama hatajuzulu chama hicho kinaelekea kufa.

"Hafai kuendelea kushika madaraka, na tunamtaka ajiuzulu wenyewe," alisema.

Naibu Katibu Mkuu wa TLP, Bw. Hamad Tao alisema wanachama wamevumilia vya kutosha vitendo vinavyofanywa na Bw. Mrema tangu amekuwa kiongozi wa chama hicho na kumtaka kuelewa kwamba uongozi umemshinda.

Bw. Tao alimtaka Bw. Mrema kuelewa kwamba TLP inaweza kuwa na maendeleo makubwa bila yeye.

"Mbona NCCR-Mageuzi inaendelea kuwepo hata sisi tunaweza kukiendesha chama bila yeye kuwepo," alisema Bw. Tao.

Bw. Tao alisema haoni haja ya Bw. Mrema kuendelea kungangania madaraka wakati ameshindwa kukiletea maendeleo chama hicho.

Mwenyekiti wa TLP Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Mhamani Lombanyama alisema wana wasiwasi na Bw. Mrema na kudai kwamba atakuwa ametumwa kuleta mvurugano ndani ya chama hicho.

Aliongeza kuwa Bw. Mrema ni lazima atambue kwamba ubunge anaojivunia hakupata kwa nguvu zake wenyewe, bali wananchi ndiyo waliomchagua.

Pia alidai kuwa anashangaa kuona kiongozi huyo, anageuza ruzuku inayotolewa na serikali kwa ajili ya chama, kuwa mali ya Jimbo la Vunjo. 

Pia alisema wanashangaa kuona kiongozi huyo amezigeuza mali za chama kuwa zake na kuzipeleka katika Jimbo lake la Vunjo.

"Amechukua pikipiki, kadi na bendera za cha TLP na kwenda kuviweka nyumbani kwake alidai," Bw. Lombanyama.

Naye Mjumbe wa Halamashauri ya chama hicho na katibu mwenezi Mkoa wa Iringa, Bw. Blanca Haule alidai kuwa Bw. Mrema hafai kuwa kiongozi wao na kumtaka akae pembeni kwa sababu alighushi katiba ya chama hicho.

3 comments:

  1. Bwana Tao na wenzako mnaotaka huyo Mzee ajiuzulu mtasaidia nini watanzania? Kazi ya mheshimiwa Mrema inaonekana wazi, acheni ubinafsi, zungumzeni mtengeneze chama kwa ajili ya uchaguzi ujao, huku mkimtumia mheshimiwa Mrema Kama nguzo yenu. Msirudie makos a yanayoendelea kufanyika kila wakati ya kupunguza nguvu za upinzani, ningependa kuona bunge lenye idadi sawia ya wabubge wa chama kitachotawala na wale wa chama vya upinzani ili kuwepo na "check and balance" katika uendeshaji bunge. Hapo ndo nchi itapiga hatua katika maendeleo.

    ReplyDelete
  2. Mtoeni huyo mzee Mwenyekiti anadhoofisha upinzani na akili imechoka na bado anafanya kazi kama yupo kwenye ofisi za upelelezi mtoeni mjipange upya.Muendeleze chama maana utafikia mwisho mbaya sana TLP na viongozi muwe mnasoma saikolojia ili kuwajua viongozi wenu

    ReplyDelete
  3. Wakimtoa huyo mzee ndiyo suluhisho? Tatizo ni ubinafsi wa Tao, hata kama kazeeka ila bado kazi zake zinaonekana waziwazi, mwachani amalize muda wake wakati mnajiandaa kumweka huyo wa kwenu ambae ni kijana, mzima, mwenye akili ambazo hazijachoka na ambae si kibaraka wa ccm. Tumieni ubongo wenu na siyo makalio kufikiria achane ubinafsi msije ua chama kwa ajili ya unafiki na ushabiki usio na tija. Mbona nyie hamkuchukua form za kugombea kama mlikuwa wasafi?? Labda nyie ni malaika, lakn kama ni binadamu kama Mrema hamna jipya ni ulafi tu mashoga wakubwa nyie

    ReplyDelete