01 July 2011

Vimwana wa Twanga pepeta watambiana

Na Addolph Bruno

WASHIRIKI wanaowania taji la 'Kimwana wa Manyele wa Twanga Pepeta' wametambiana kutwaaa taji hilo litakalofanyika Julai 8, mwaka huu katika Ukumbi wa
Ubungo Plaza, Dar es Salaam.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na waandishi wa habari Dar es Salaam juzi, katika kambi yao ya mazoezi kila mmoja alisema wanajiamini kutokana na uzoefu wao wa kucheza walioupata tangu kuanza kujiandaa.

Mmoja wa vimwana hao, Johari Juma alisema anaamini atanyakua taji hilo kutokana na uzoefu alionao pamoja na kuuelewa vyema udhaifu wa wanzake wakiwa jukwaani.

"Mimi Johari Juma, kimwana wa ukweli nawakaribisha Watanzania wenzetu wapenda burudani waje kwa wingi katika shindano letu pale Ubungo Plaza, wamshuhudie kimwana wao Johari," alitamba.

Naye Lightness Mshana, alisema amejiandaa vyema kuhakikisha anashinda katika mashindano hayo ili aweze kumiliki duka la vipodozi ambalo mshindi atazawadiwa.

Awali Mkurugenzi wa African Stars Entertainment Tanzania (ASET) inayomiliki bendi ya Twanga Pepeta, Asha Baraka alisema maandalizi yanaendelea vizuri na kwamba kila kitu kinakwenda vizuri kinachosubiriwa ni muda kufika.

Asha alisema mshindi wa kwanza anatarajia kuzawadiwa duka la vipodozi lenye thamani ya sh. milioni tano, ambalo limelipiwa kodi ya mwaka mzima, wa pili atapewa sh. 500,000, wa tatu atapata sh. 300,000 wakati wa nne hadi wa kumi watapa kifuta jasho sh. 100,000 kila mmoja.

Alisema fainali hizo zitasindikizwa na burudani mbalimbali kutoka kwa vimwana wenyewe, ambapo pia msanii wa muziki wa kizazi kipya AT, atatumbuiza na pia Twanga Pepeta itakuwa na shughuli pevu siku hiyo.

No comments:

Post a Comment