24 June 2011

Villas-Boas aahidi kumpa raha Abramovich

LONDON, England

KOCHA mpya wa Chelsea, Andre Villas-Boas amesema amejipanga kufanya makubwa yatakayomfanya mmiliki wa timu hiyo, Roman Abramovich kuwa mwenye
furaha.

Msimu uliopita kocha huyo mpya wa Blues, alitwaa mataji manne akiwa na timu ya FC Porto na kwa mujibu wa gazeti la The Sun, Villas-Boas alitangaza jana kwamba anaamini atatimiza matakwa ya Chelsea na anatarajia kuelekeza nguvu zake kutwaa mataji manne, kama alivyofanya kabla ya kutua katika timu hiyo.

"Najiamini naweza kutimiza matarajio ya  Chelsea na tunaweza kuelekeza jitihada zetu kutwaa mataji manne kama tulivyowahi kufanya," alisema.

"Nina matumaini makubwa mno na imani kwamba watu wangependa iwe hivyo. "Huu ni uongozi mpya, njia mpya niliyoingia, lakini nadhani mwisho wa yote inahitajika motisha na ni lazima kila mtu ajisikie kuendeleza ushindi wa klabu," aliongeza.

Villas-Boas (33), ambaye amesaini mkataba wa miaka mitatu na timu hiyo ya Stamford Bridge alisema, lakini anafahamu kushindwa kutwaa ubingwa wa Klabu Bingwa Ulaya ni sawa na kukalia kiti moto ndani ya Chelsea.

Carlo Ancelotti ndiye kocha wa mwisho kutimuliwa na klabu hiyo mwezi uliopita, ikiwa ni takribani mwaka mmoja baada ya kutwaa mataji mawili.

No comments:

Post a Comment