24 June 2011

Vigogo watakaokwepa kodi Kenya kufilisiwa

NAIROBI,Kenya

MAMLAKA ya mapato nchini Kenya (KRA)imesema kuwa itapiga mnada mali zote za wabunge na vigogo wa serikali watakaokaidi kulipa kodi ya mapato.Mbali na
kupiga mnada mali,mamlaka hiyo imesema kuwa pia itataifisha akaunti na fedha mali ya vigogo hao.

Taarifa hiyo ilitolewa jana na mamlaka hiyo ambapo ilisema kuwa  hatua hiyo imechukuliwa ili kuondoa kasumba ya kutokuwepo ulipaji kodi kwa fedha za wabunge  wakati wanaingiza fedha nyingi jambo ambalo limekuwa likilalamikiwa na wengi.

Inaelezwa kuwa katika posho za wabunge, wao ulipa kodi katika posho ya likizo ambayo ni sh. 200, 000  kati ya  Sh.850,000 za masulufu  wanayopokea.

Vigogo wengine wanaotajwa kuwemo katika mkubo huo wa walipa kodi ni,mwanasheria mkuu,majaji,mdhibiti na mkaguzi mkuu wa fedha za serikali,mwenyekiti na wajumbe kamishna wa huduma za umma,mwenyekiti na wa wajumbe wa tume huru ya uchaguzi.

Katiba ya Kenya inatoa amri kwa kila ofisa yoyote  kulipa kodi na tangu ipitishwe rasmi kuwa sheria Agosti 27 mwaka jana kipato cha maofisa wa Serikali ni lazima kikatwe  kodi.

Kutokana na hali hayo,Kamishna wa Mamlaka ya mapato ya ndani, Bw.John Njiraini anasema kuwa  KRA imewapa maofisa na waajili muda  hadi katikati ya mwezi ujao kuwa wamelipa kodi zao na akasema kuwa endapo watakaidi hatua zitachukuliwa ili kufidia fedha hizo.

Hata hivyo mtoza kodi huyo alisema kuwa hatarajii kama suala hilo litafikia hatua hiyo bali zitapatikana njia mbadala ili kumaliza suala hilo.

 “Hatua nyingine tunayoweza kuchukua kufidia fedha ni kupitia akaunti ya mtu binafsi  . Ila tunatarajia utapatikana  ufumbuzi wa suala hili,”alisema kamishna huyo.

Naye Naibu Spika wa  Bunge,Bw.Farah Maalim alipongeza hatua hiyo ya  kutozwa kodi akisema kuwa hakuna jinsi zaidi ya kufanya hivyo kutokana na kuwa sheria ipo wazi haiwapi msamaha wa kutolipa kodi.(Daily nation).

No comments:

Post a Comment