29 June 2011

Utamaduni wa Tanzania kivutio China

Na Amina Athumani

WATU wa China wamevutiwa na utamaduni wa Watanzania katika tamasha la tatu la utamaduni lililoanza jana nchini China.Katika tamasha hilo, Tanzania inawakilishwa na
Mwenyekiti wa Chama cha Michezo ya Jadi (CHAMIJATA), Mohamed Kazingumbe ambaye anautangaza utamaduni huo.

Kutokana na hatua hiyo, watu hao wa China pamoja na Japan wamevutiwa kuja nchini kushiriki mashindano ya taifa ya Jadi yatakayofanyika Agosti mwaka huu, ili kujionea utamaduni wa Tanzania.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana na Kazingumbe, ilieleza kuwa kuwaleta watu wa China inawezekana endapo kama serikali itagharimia mashindano hayo.

Kazingumbe alisema tamasha hilo, litakuwa la siku tatu ambalo lilianza jana na yeye ameweza kunadi sera za CHAMIJATA ili kutafuta wadau wa kujenga ushirikianao katika kuinua michezo ya jadi.

Mwenyekiti huyo alisema mbali na kutoa sera mbalimbali za utamaduni wa Tanzania, pia akiwa huko atasoma mengi kutoka nchi washiriki, ili iwe nguzo katika kuimarisha chama chake na michezo ya jadi nchini.

"Hata hivyo nitawasiliana na serikali, kuona kama tunaweza japo kuwakaribisha kwetu waone mashindano yetu kwa gharama zao, wenzetu wana uwezo wangefurahia jambo hilo," alisema Kazingumbe.

Alisema tamasha hilo la China linajulikana kama 'Ginghai Ledu Traditional Archery Competition' na linafanyika katika mji wa Ledu uliopo katika Jimbo la Ginghai na linashirikisha nchi 40 Duniani.

No comments:

Post a Comment