Na Mwandishi Wetu
MASHINDANO ya Miss Kinondoni 2011, yamezinduliwa juzi rasmi na leo washiriki 15 wanatarajia kuingia kambini Mzalendo Pub kwa ajili ya kujiandaa na fainali
hizo.
Akizindua mashindano hayo Dar es Salaam juzi, Mwenyekiti wa Kamati ya Miss Kinondoni Yusuf Omary 'Boy George', aliwapa washiriki hao misingi, kanuni na sheria za michuano hiyo.
"Katika mashindano haya ya urembo hakuna upendeleo hata kidogo, maana nasikia katika mashindano ya vitongoji kuna washiriki walilia wakidai kuna upendeleo unafanyika, kitu kama hicho hakipo," alisema.
Aliwataka washiriki hao kuwa na nidhamu ndani na nje ya mazoezi katika kipindi chote cha kujiandaa na mashindano ya Miss Kinondoni ili kuepuka kuchafua heshima ya michuano hiyo ya urembo.
Alisema anawahakikishia kwamba mashindano ya urembo si uhuni kama inavyotazamwa na baadhi ya watu, hivyo amewataka washiriki hao kuhakikisha wanakuwa na juhudi katika mazoezi yao ili waje kufanya vyema siku ya mwisho.
Mwenyekiti huyo alisema washiriki hao watafunzwa na Miss Kinondoni 2007 ambaye pia alikuwa Miss Tanzania mwaka huo, Richa Adhia na katika muziki watakuwa chini ya Sammy Cool.
Washiriki hao awali kabla ya kuingia fainali ya Miss Kinondoni, walishiriki katika ngazi ya vitongoji vya Sinza na Dar Indian Ocean.
Warembo wanaotarajia kuwania taji hilo la Kinondoni ni Pamela Mapango, Stela Mbuge, Felister Philip, Stela Moris, Naomi Jones, Husna Maulid, Catherine Frisch na Mariam Almas.
Wengine ni Fatma Pongwa, Stela Premsingh, Hamisa Hassan, Zainab Akonina, Sabrina Abdallah na Winnie Gerald. Mashindano hayo yanadhaminiwa Redd's, Vodacom na Ppapa-Z.
No comments:
Post a Comment