RIO DE JENEIRO, Brazil
RAIS wa Klabu ya Santos, Luis Alvaro de Oliveira Ribeiro amethibitisha kuwa klabu tano Ulaya zimekubali kulipa dau la euro milioni 45 kwa ajili ya
kunasa saini ya Neymar.
Kauli ya rais huyo imekuja wakati kuna tetesi zilizosambaa zikieleza kuwa timu za Real Madrid, Barcelona, Chelsea, Manchester City na klabu kutoka Russia, Anzhi Makhachkala kuwa katika mvutano wa kumwania nyota huyo.
"Hatutaki kumuuza mchezaji huyo, lakini kuna uwezekano wa kulipwa fedha za kutengua mkataba," alisema kwa mujibu wa ESPN Brasil.
"Klabu kubwa tano Ulaya zimeshatoa ofa ya kutengua mkataba. Siwezi kuzitaja kwa sababu kuna makubaliano kati ya Santos na klabu hizo, lakini ni klabu muhimu Ulaya," alisema rais huyo.
Alisema klabu hizo kwa kutumia maadili ziliwafuata viongozi wa Santos na kueleza nia yao ya kutaka kulipa fedha hiyo na hivyo wakatoa idhini kwa kila klabu kufanya mazungumzo binafsi na baba mzazi wa Neymar ambaye ni wakala wake, Wagner Ribeiro ama mwakilishi yeyote wa mchezaji huyo.
Klabu ya Chelsea ndiyo inaonekana kukataliwa mara nyingi ofa zake za kutaka kumsajili Neymar, kabla Mbrazil huyo mwenye umri wa miaka 19 hajasaini mkataba wa muda mrefu na klabu hiyo.
Taarifa hizo zimekuja siku moja baada ya Ribeiro, kusema Neymar anataka kuwa mchezaji bora duniani wakati akiwa Brazil na akasema ana imani mchezaji huyo ataendelea kubaki Santos.
No comments:
Post a Comment