30 June 2011

Usiku wa za Kale ni Dhahabu waja Julai 7

Na Mwandishi Wetu

KAMPUNI ya Mac D Promotion, imeandaa onesho la Usiku wa za Kale ni Dhahabu litakalofanyika katika Julai 7 mwaka huu kwenye Ukumbi wa
Mzalendo Pub Jijini Dar es salaam.

Akizungumza Dar es Salaam jana Ofisa Uhusiano wa Mac D Promotion, Peter Mwendapole alisema usiku huo
utapambwa na mwanamuziki nguli nchini, Kikumbi Mwanza Mpango 'King Kiki' na kundi zima la La Capital 'Wazee Sugu'.

Alisema katika onesho hilo, Wazee Sugu watapanda jukwaa moja na wakongwe wengine wa
muziki wa dansi nchini Tshimanga Asossa na Kasongo Mpinda 'Cleyton', ambao wamedhamiria kuwasha moto Mzalendo Pub kwa mara ya kwanza.

Mwendapole alisema katika onesho hilo zitapigwa nyimbo zote kali za enzi hizo ikiwa
ni pamoja na Nimepigwa Ngwala, Kitambaa Cheupe, Angelou, Seya, Kibela Acha
Chuki, Ishara ya Mapenzi, Huba, Fransisca na nyinginezo.

Alisema wanamuziki hao hivi sasa wapo katika mazoezi makali kuhakikisha usiku huo
uliodhaminiwa na Bandawe Freight Tanga, Double View Hotel, Sk Bake Place, DenFrance Hotel, Screen Masters na Florida Executive Inn unakuwa wa kusimuliwa na kiingilio ni sh. 5,000 ili kila mmoja aweze kumudu
kwenda kuufurahia usiku huo.

Mwendapole alisema maandalizi ya onesho hilo ambalo linafanyika kwa mara ya kwanza jijini Dar es salaam, yamekamilika na kuwataka wakazi wa Dar es Salaam kutokubali kupitwa na usiku huu ambao utakuwa ni wa kukumbukwa.

No comments:

Post a Comment