30 June 2011

Andy Cole awapa mbinu Makongo

Na Addolph Bruno

MSHAMBULIAJI wa zamani wa Manchester United na timu ya taifa ya Uingereza, Andy Cole amewataka vijana wanaochipukia katika soka nchini kuwa wasikivu kwa makocha
wao na kuzingatia mazoezi ili kufikia malengo yao.

Cole aliyeichezea klabu hiyo miaka 7 na kutwaa ubingwa mara 5, aliwasili nchini jana akitokea Kenya na baadaye kuzindua programu maalumu ya soka inayodhaminiwa na Kampuni ya simu za mkononi Airtel.

Programu hiyo inayofahamika kwa jina la Airtel Rising Stars inajumuisha Afrika nzima kutoa nafasi kwa wanasoka chipukizi na lengo lake ni kuibua na kuviendeleza kuanzia ngazi ya chini hadi taifa, ambapo wanafunzi watakaofanya vizuri watajifunza soka katika shule za soka, zinazomilikiwa na Man United.

Akizungumza Dar es Salaam jana, kabla ya kuzindua programu hiyo iliyofanyika katika Uwanja wa Shule ya Sekondari Makongo na kushirikisha wanafunzi wa shule hiyo, Cole alisema amefurahi kukutana na wanafunzi hao na kuwasisitiza kuwa wasikivu.

"Na mimi nimefurahi kuungana na Airtel katika mapango huu mzuri, nafikiri sote tukifanya vizuri tutafanikisha malengo yetu na pia ninaamini wachezaji wengi wazuri watatoka Afrika na kuungana na Manchester United, katika kuifikisha soka mbali," alisema.

Awali Cole, ambaye aliambatana na mwakilishi kutoka Manchester United, Nicky Humphrey aliwataka wachezaji hao kuzingatia maelekezo ya makocha na kufanya mazoezi kwa bidii, ili kufanikiwa.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania, Sam Elangalloor awali alisema kampuni yake imejikita kuwekeza katika soka kutokana na mchezo huo kuleta mshikamano kwenye jamii na kutoa fursa ya mamia ya wachezaji kuendesha maisha yao katika kiwango cha juu.

Alisema Airtel itaendelea kufanya kazi karibu na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo pamoja na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ili kutekeleza programu hiyo kwa wasichana na wavulana.

Kwa upande wake Naibu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dkt. Fenella Mukangara alisema program hiyo inaongeza msukumo kwenye mpango wa maendeleo ya soka nchini na kupongeza ubunifu uliofanywa na kampuni hiyo.

No comments:

Post a Comment