29 June 2011

Uagizaji mafuta pamoja kupunguza bei-UWURA

Na Agnes Mwaijega

MAMLAKA ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) imesema inajipanga kuanzisha mfumo mpya utaoziwezesha kampuni zote kuagiza na kusafirisha mafuta kwa
pamoja ili kukabiliana na ushindani kimataifa.

Pia imesisitiza kuwa itaendelea kudhibiti kampuni zote zinazosafirisha mafuta bila kulipa kodi.

Akizungumza katika mkutano wa wadau mbalimbali wa mafuta Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa EWURA, Bw. Haruna Masebu alisema sheria ya kusimamia mfumo huo iko tayari kinachosubiliwa ni utekelezaji wa kampuni ambao unatakiwa kutekelezwa ndani ya miezi mitatu ijayo.

Aliseama mfumo huo utasimamiwa na wafanyabiashara wa mafuta na utawasaidia kupata mafuta kwa bei nafuu.

Aliwataka wadau kuanzisha bodi kwa ajili kuanza utekelezaji wa mpango huo.

Aliongeza kuwa EWURA itazingatia uwazi katika utendaji ili kuhakikisha mfumo huo unaleta mafanikio.

Pia alisema punguzo la kodi ya mafuta katika mamlaka hiyo utazingatia punguzo lililowekwa na serikali.

Pia aliiunga mkono serikali kwa kuongeza kodi ya mafuta ya taa na kusema kuwa itasaidia kupunguza uchakachuaji uliokuwa umeshakithiri.

"Tofauti ya kodi kati ya diseli na petroli ni ndogo sana, ni dhahiri kwamba sasa uchakachuaji utakuwa umepatiwa ufumbuzi," alisema.

1 comment:

  1. Tuone hatua hizi zinamletea nafuu, mtanzania na kuboresha uchumi wa taifa

    ReplyDelete