29 June 2011

Mbunge: Watendaji wanamdharau rais

Na Grace Michael, Dodoma

WABUNGE wameendelea kuirarua serikali katika mjadala wa bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kuhusu mambo mbalimbali hasa utendaji wake na baadhi wakienda mbali
wakisema kuwa wapo watendaji wanaomdharua Rais Jakaya Kikwete.

Miongoni mwa wabunge hao ni Bw. Salum Baruany (Lindi Mjini-CUF), aliyesema kuwa kutotekelezeka kwa ahadi za Rais Kikwete katika maeneo mbalimbali nchini ni dalili kwamba watendaji kumdharau rais wao.

“Ahadi za rais si ahadi za kufanyia mchezo kwa kuwa kauli yake ni nzito na huwa ni ya mwisho, lakini pia kauli yake inaizidi hata sheria. Lindi alikuja na kuahidi mambo mengi ikiwemo bandari, soko na nyingine nyingi, na sasa amebakiza
miaka mitatu kumaliza mkataba wake wa urais na hakijafanyika chochote na hii inaonesha au ina maana kuwa serikali  mnamdharau rais wenu,” alisema.

Alisema kuwa kuna mambo mengi ya kimaendeleo ambayo yamekwama na kusababisha nchi kushindwa kupiga hatua kutokana na watendaji kutowajibika.

Mbunge huyo alisema kuwa wananchi kila kona wanalalamikia mambo mbalimbali yakiwemo ya ajira ambazo alieleza kuwa zimeghubikwa na kujuana na ukabila.

“Mfano mzuri ni kwenye kada ya majeshi yetu, ajira za polisi na majeshi mengine kwa sasa zinapatikana kwa kujuana, mtu akiwa RPC sehemu fulani anaita ukoo wake wote na hii tusipoangalia italeta hatari hapo baadaye,” alisema.

Suala jingine alilozungumzia ni tatizo la mauaji ya albino, ambapo aliitaka serikali kutoa tamko ni hatua gani zilizofikiwa na serikali katika kukomesha tatizo hili na kudhibiti tatizo jingine ambalo lipo sasa la walemavu hao kupotea katika mazingira ya kutatanisha.

Mbunge huyo ambaye pia ni albino, alisema kuwa dalili zinaonesha kuwa biashara hiyo haramu ya viungo vya albino, ilikuwa inafanywa na watu wenye uwezo mkubwa kwa kuwa viungo hivyo viliuzwa kwa gharama kubwa kama sh. milioni 200 hadi 400.

Alisema kuwa kiwango hicho cha fedha kisingekuwa rahisi kwa watu wenye uwezo wa chini, hivyo akashauri ni vyema ukafanyika utafiti kubaini watu hao, huku akiomba kundi la walemavu kuingizwa katika wizara mtambuka na si kubaki katika Wizara ya
Afya na Ustawi wa Jamii.

Naye Mbunge wa Jimbo la Kasulu Mjini, Bw. Moses Machali, alisema kuwa pamoja na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi kujisifu kuwa imefanya mambo makubwa ndani ya kipindi cha miaka 50 ya uhuru, lakini alisema yaliyofanywa hayalingani na
kipindi hicho.

Alisema kuwa inashangaza kuona nchi ya Tanzania ikigeuka kuwa ombaomba na ikiachwa nyuma na nchi zingine ambazo kwa kipindi cha nyuma ukuaji wake wa uchumi ulikuwa ukienda sambamba ambapo alitolea mfano wa China ambayo kwa sasa uchumi wake umeimarika na Tanzania inaomba misaada huko.

Akizungumzia suala la amani ambalo serikali imejivunia kuilinda, alisema kuwa kamwe nchi hii kwa sasa haina amani kwa kuwa inakabiliwa na matatizo mengi kama ya njaa, ukosefu wa ajira, watu kujichukulia sheria mkononi kutokana na serikali
kushindwa kufanya maamuzi na kutokuwepo na haki.

“Tusijidanganye kuwa tuna amani, hatuna amani bali tuna utulivu ambao unaambatana na woga, na kama serikali inataka nchi iwe na amani ya kweli basi isikilize wananchi wanachokitaka na ikitekeleze,” alisema Bw. Machali.

Alisema kuwa hata kwa upande wa wabunge ambao jukumu lao kubwa ni kuwawakilisha wananchi na kuisimamia serikali, wameacha jukumu hilo na wamekuwa upande wa wasemaji wa serikali, hivyo kutowatendea haki wananchi.

Akizungumzia kushuka kwa nidhamu ya kazi kwa watendaji serikali na kukosekana kwa uwajibikaji, alisema kuwa ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali ni ushahidi tosha wa kuwachukulia hatua watendaji ambao wameonekana kutofanya vizuri katika maeneo yao na kupoteza fedha za serikali.

“Mfano, juzi mbunge wa Mvomero, Amos Makalla alituambia hapa bungeni kuwa Mkuu wa Wilaya amewanyima wananchi chakula cha msaada, na huu ni mfano tosha wa kutokuwepo kwa uwajibikaji kwani mtu kama huyu katika nchi zingine anapigwa risasi lakini hapa kwetu akiharibu Kasulu anapelekwa Kigoma,” alisema.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Nyamagana, Bw. Ezekiel Wenje ambaye alianza kwa kuweka msimamo wake kuhusu kuondolewa kwa posho za vikao, alisema hata leo yeye na wenzake wa CHADEMA wako tayari kutosaini fomu ya posho endapo itatenganishwa na ya mahudhurio.

Akizungumzia suala la amani, Bw. Wenje alisema kuwa hakuna sababu ya kuwahadaa wananchi kuwa kuna amani wakati wananchi wanakosa haki.

Alisema kuwa amani inavurugika kwa kuwa haki za wananchi zinaporwa bila sababu ya msingi na akatoa mfano wa kipindi cha kutangazwa majina ya washindi katika uchaguzi mkuu mwaka jana, ambapo alisema kuwa bila wananchi kujitoa mhanga na kuwa tayari kupoteza hata uhai wao, baadhi ya wabunge wasingetangazwa kuwa washindi.

“Mfano mdogo ni jimboni kwangu, mtu nimeshinda lakini kutangazwa tu ilikuwa ni shida, hivyo vitendo vya kuchukua haki za watu si kizuri na sisi wapinzani tutaendelea na msimamo wetu wa kuandamana ili kudai haki hizi zinazopotea na
hata kesho tutaandamana,” alisema.

Alishangaa tamko ya Waziri wa TAMISEMI, Bw. George Mkuchika ambaye alijisifu kuwa ubadhilifu wa fedha za serikali umepungua kwa kuwa hata ripoti ya CAG hati chafu zimepungua.

“Nilitarajia kumsikia waziri aseme kuwa wakurugenzi ambao halmashauri zao zimepata hati chafu wamefukuzwa na wenye hati za mashaka wako katika uangalizi, lakini serikali yetu inachokifanya kwa watendaji wabovu ni kuwahamisha kutoka
eneo moja kwenda jingine,” alisema.

Bw. Wenje pia alionekana kukerwa na na uporwaji wa ardhi unaofanywa na serikali na watu wengine jimboni mwake ambapo alisema bila suala hili kushughulikiwa litasababisha matatizo hapo baadaye.

“Haiwezekani mwananchi amezaliwa hapo na kukulia hapo, pengine ana ekari nane na yuko na watoto wake...leo manispaa inasema inapima viwanja na inachukua eneo hilo na kumwachia ekari moja huku ikimtaka alipie sh. milioni moja na nusu, huku ekari zingine amefidiwa kwa laki nne kila ekari...hii haiwezekani, na sitakubali,” alisema.

2 comments:

  1. Haya yote mnayajua Viongozi wa Tanzania wanakuwa wakarimu sana wanapogombea uongozi lakini pindi ndoto zao zinapo fanikiwa hugeuka na kuwa mithili ya KOBRA hawataki kusikiliza matatizo ya wananchi wao, Mfano mwenye pesa hafungwi,Mahakama imewekwa kutoa haki lakini kwao ni kitega uchumi,Polisi wa kulinda amani wao wanakubambikia kesi na viongozi wanayajua haya Lakinikama watajiwekea uzalendo wa kusikiliza kero za wananchi bila kujali itakadi zao za maisha itasaidia sana mfano mtu anakuwa usumbufu wizara fulani maana watunza mafaili wanasumbua mturuhusu kumuona waziri au katibu kushtaki uzembe unaoendelea hapo na pia mahakamani au polisi Lakini cha kushangaza hutopata nafasi hiyo kisingizio huna Appointment au mwambie sipo. jamani siyo kila mtu anayetaka kuwaona anakuja omba pesa na kama ni hivyo mwambie sina na aondoke lakini wekeni misingi ya kukutana na yeyote ambae ataomba akuone, kwani watu kujiweka kama mitume au miungu watu inawasaidia nini wakati kuna siku utakufa tu na kuyaacha yote hayo huo ni ulimbukeni mbona nchi za wenzetu kama Scandnavia kumuona kiongozi ni rahisi sana hata sisi wahamiaji hutuna matatizo kama huko kwetu inashangaza sana kuona watu mmeenda shule lakini hamuendani na wakati si balaa hil.

    ReplyDelete
  2. Unatagemea nini ikiwa Rais mwenyewe ni "mtoto wa mjini". Ni lazima mawaziri na watandeji wake wafanane naye. Nafikiri kinachoendelea TZ ni designer suits za Rais na mawaziri wake. Hakuna leadership wala vision toka juu, sasa unategemea nini.

    ReplyDelete