Na Mwandishi Wetu
MAMIA ya mashabiki walijimwaga na kuserebuka kwenye Klabu ya Mbalamwezi Beach, Dar es Salaam kushiriki kwenye tamasha la Str8Muzik Beach Party 2011 lililofanyika
juzi na kuburudishwa na mwanamuziki wa kimataifa kutoka Jamaica, Elephant Man aliyekonga nyoyo za mashabiki.
Nyota huyo mwimbaji wa muziki wa Dancehall Reggae, Elephant Man ambaye hujulikana kama Energy God (Mungu wa Nguvu) alipanda jukwaani dakika chache baada ya kutimia saa nne usiku na kutoa shoo ya nguvu, akiwaacha mashabiki wakijimwaga kwa kukata nyonga.
Elephant katika burudani hiyo, alihakikisha anawapa raha ya uhakika mashabiki waliofika katika onesho hilo, huku akiisifia Tanzania jinsi ilivyokuwa nzuri lakini akisisitiza kwamba anapiga muziki kwa ajili ya Dunia.
"Afrika ni nzuri, Tanzania ni kubwa, kuna vimwana wa ajabu wa Kiafrika," alikuwa akifoka foka hivyo mara kwa mara.
Msanii huyo licha ya kuimba dancehall reggae, pia aliimba na kucheza katika miondoko tofauti, ikiwa ni pamoja na sweet reggae, dance reggae na mchanganyiko wa slow sweet reggae.
Pia aliimba wimbo wa Michael Jackson wa 'We are the World', lakini alifanya hivyo katika aina ya pekee ya sweet reggae, akihitimisha makamuzi yaliyodumu kwa saa moja nusu.
Matukio yote hayo ya ufukweni yaliyoanza asubuhi hadi jioni na kushirikisha wasanii wa Tanzania na Kenya, waliokuwa wakifanya maonesho ya utangulizi, kabla ya msanii huyo kupanda jukwaani.
Wanamuziki waliotangulia kwenye onesho hilo ni pamoja na washindi wa tamasha la Stre8Muzik Freestyle 2011 Cpwa, Fid Q, P-Unit na Red San kutoka Kenya.
Str8Muzik Beach Party 2011, iliandaliwa na Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC) kupitia chapa yake ya Sweet Menthol.
No comments:
Post a Comment