28 June 2011

Tevez, Man City waingizwa katika skendo

LONDON, Uingereza

CARLOS Tevez na Manchester City wameingizwa katika skendo ya upangaji matokeo. Wakati hakuna mawazo kama mchezaji au klabu  imefanya makosa, mahakama ya
Ugiriki inachunguza ushahidi kwamba mechi ya Ligi ya Europa dhidi ya Aris iliyochezwa Februari mwaka huu ililengwa kutumiwa na wacheza kamari.

Waendesha mashitaka waliwasilisha mahakamani mazungumzo ya simu, ambayo anasikika mmoja wa wachezaji wa timu ya Ugiriki akidai kuwa watawasiliana na Tevez kusaidia.

Kiungo wa timu ya Aris, Kostas Mendrinos alisikika akisema atamwomba mchezaji mwenzake wa zamani wa City, Nery Castillo amwambie Tevez kuachia timu ya Ugiriki.

Inaaminika katika kamari hiyo karibia pauni 6,000 ziliwekwa.

Mendrinos alisema: "Ninazungumzia uwezekano na Castillo kwenda na kuwasiliana na Tevez, ambaye ni nahodha na pia tutamwambia Koke (nahodha wa Aris) pengine tuanze sisi kucheza."

Mazungumzo yaliyorekodiwa yamejitokeza baada ya polisi wa siri kupata simu kutoka kwa wachezaji na maofisa wa klabu, wakilalamika uwezekano wa kuwepo kwa upangaji wa matokeo.

Tevez juzi alikanusha kuhusu jambo hilo au kuhusika kwa namna yoyote.

Msemaji wake alisema: "Haiwezekani. Carlos hajawahi kusikia kitu kama hicho na hakuna mtu aliyewasiliana naye."

Na City juzi usiku ilisema Tevez na Castillo hawajawahi kucheza pamoja ambapo kipindi cha mkopo cha mchezaji kutoka Mexico aliyecheza England kiliisha mwaka mmoja kabla ya Tevez wa Argentina kuondoka Manchester United kuhamia Eastlands.

Mahakama inachunguza ni kwanini wachezaji wa Aris, walijihusishwa na kamari ya kutabiri.

Nahodha huyo wa Aris, Koke, anayetajwa katika tepu, hakucheza huku kipa Michalis Sifakis alichukua nafasi yake.

Ingawa katika upigaji kura ya timu kabla ya kuanza mpira ni Sifakis alishinda, City ilianzisha mpira katika mechi iliyoishia kwa matokeo ya 0-0.

No comments:

Post a Comment