28 June 2011

Ali Kiba apata ajali Mikumi

Na Stella Aron

WANENGUAJI wawili wa msanii wa kizazi kipya, Ali Kiba wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, baada ya gari walilokuwa wakisafiria
kupinduka.

Gari hilo ambalo pia msanii huyo alikuwemo amenusurika kufariki katika ajali hiyo wakati wakitokea Mkoani Mbeya.

Akizungumza kwa njia ya simu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Adolphina Chialo alisema ajali hiyo ilitokea juzi saa 11 alfajiri katika eneo la Mikumi mbugani.

Kamanda Chialo alisema gari hilo, lenye namba za usajili T 523 BQB aina ya Toyota lilikuwa na abiria watano ambapo lilikuwa likiendeshwa na dereva aliyefahamika kwa jina la Said Haruna (30), mkazi wa Magomeni jijini Dar es Salaam.

Amewataja wasanii waliokuwemo kuwa ni Ally Saidi (24), Emmanuel Elias (20), Hashiri Abdulaziz (20), wote wakazi wa Kariakoo, Sidney Msafiri (20), mkazi wa Tandale na Issa Shabani (19), mkazi wa Sinza.

Kamanda huyo alisema kuwa katika ajali hiyo abiria wawili walijerihiwa vibaya, ambao ni Issa Shababi na Hashiri na wamelazwa katika hospitali ya Mkoa.

Alisema chanzo cha ajali hiyo ni baada ya usukani kumshinda dereva na kusababisha gari hilo kupinduka.

Hata hivyo baadhi ya wasanii, ambao hawakupenda kuzungumza na gazeti hili walidai kuwa walikuwa wakiwahi ndege ya saa tano asubuhi jijini Dar es Salaam, ili kwenda Mbeya kwenye onesho la Fiesta.

No comments:

Post a Comment