27 June 2011

Shibuda awashukia vikali mawaziri wa Rais Kikwete

Na Rashid Mkwinda,Dodoma

MBUNGE wa Jimbo la Maswa Magharibi (CHADEMA) Bw.John Shibuda, amesema utendaji mzuri wa Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda, unavurugwa na baadhi ya
mawaziri aliodai ni mzigo  ambao hawana utashi na ari ya kuwatumikia wananchi na taifa kwa ujumla.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili mjini hapa,  Bw.Shibuda  alisema Bw. Pinda  ana wakati mgumu katika kipindi cha uongozi wake kutokana na watendaji wabovu wasioitakia mema nchi.

Alisema uwajibikaji ni sera nzuri iliyoasisiwa na Baba wa Taifa Marehemu Mwalimu Julius Nyerere, lakini viongozi waliopo wanatumia msemo huo kama wimbo ambao wanashindwa kuutekeleza kutokana na kugubikwa na ubinafsi.

"Baadhi ya wasaidizi wa huyu  mtoto wa mkulima  ni mzigo kwa taifa letu, hawafai kabisa kuwa viongozi walipaswa kufukuzwa na kuondolewa katika uongozi..hawana nia njema na nchi yetu,"alisema Bw.Shibuda na kuongeza;

"Nchi hii inatakiwa kuongozwa na viongozi waadilifu wenye utashi na uchungu na nchi yetu,"alisema Bw. Shibuda.

Alifafanua kuwa baadhi viongozi  kuanzia wakuu wa wilaya, wakuu wa mikoa,mawaziri na watendaji wengine serikalini walipaswa kutimuliwa uongozi kwa kuwa hakuna wanachokifanya.

Alisema kuwa bashasha ya waziri mkuu inapotea siku hadi siku, kutokana na kugubikwa na mawazo ya ugumu wa kazi zinazomkabili mbele yake kwa kuwa baadhi ya wasaidizi wake wamemtupia  majukumu  peke yake.

Akitolea mfano kauli hiyo Bw.Shibuda alisema kuna sera ya Kilimo Kwanza iliyorithiwa kutokana na falsafa za  Kilimo ni Uti wa Mgongo ,  Siasa ni Kilimo na mengineyo mfano wa haya, lakini hakuna hata kiongozi mmoja ndani ya CCM ambaye anamuunga mkono waziri mkuu katika kupigania
wakulima hali inayomfanya muda wote kukosa raha.

"Suala hili la kilimo limetelekezwa kwa Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu Bw.Pinda, wengine ni propaganda kisiasa, wanachokijua ni  kupiga vita maandamano ya CHADEMA," alisema na kuongeza kuwa, wakulima wanataka kusikia maneno yenye tija kuhusu kukosekana kwa pembejeo za kilimo,na namna ambavyo serikali imejipanga kuwapatia wakulima pembejeo kwa njia rahisi.

Akitolea mfano wa ziara za CCM zinazofanywa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Bw.Nape Nnauye, kwamba zimelenga kuendelea kuwapumbaza wananchi juu ya kile kinachozungumzwa kuwa wapo viongozi mafisadi ambao hata hivyo hawachukuliwi hatua za kisheria zaidi ya
kuzungumza majukwaani.

Bw.Shibuda ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya Bunge Mambo ya Nje,Ulinzi na Usalama alisema kuwa iwapo zingefuatwa sheria kama zile zinazofuatwa  China na kwingineko,watu hawa wangepigwa risasi na kutoweka kabisa duniani na suala la kuzungumzia ufisadi lingekoma na kugeuka historia  kwani hakuna mtu ambaye angethubutu kuhujumu mali za wavuja jasho.

Alisema ziara za CCM kwa wananchi hazigusi matatizo yatokanayo na ukosefu wa pembejeo na jinsi serikali ilivyojipanga kupatia ufumbuzi tatizo la wakulima, bali kinachozungumzwa ni propaganda za kukipiga vita CHADEMA kutokana na jitihada zake za kuwaamsha wananchi kujua
mustakabali wao.

8 comments:

  1. VIVA SHIBUDA, WEWE NI MPAMBANAJI HALISI ACHA HAO WANAONG`ANG`ANIA VYAMA HATA KAMA HAVINA TIJA KWA WANANCHI
    BRAVO SHIBUDA

    ReplyDelete
  2. SHIBUDA ndiye aliyevua GAMBA, hawa wengine ni blablabla. Wabunge wa CCM hawawezi pitisha sheria ya kupigwa risasi hadharani wale wanaohujumu Taifa maana watamalizika wenyewe wote na kuzomeazomea kwao mambo ya Msingi bungeni badala yakuanzalia maslahi ya Taifa.

    ReplyDelete
  3. Mtu kama huyu Shibuda ni hatari yeye anaona wanachofanya CHADEMA ndo sawa , ila wanachofanya CCM sio . Huu ni mtazamo wake na lazima atambue kuna tofauti kubwa kati ya vyama hivi kwa kuwa CDM wanachosema si wanachotekeleza na mfano ni bajeti yao mbadala ambayo haiendani na ilani yao ya uchaguzi.

    so hakuna mtu wa kukubali hizo propaganda , mpaka 2015 hakuna CHANDIMU .

    ReplyDelete
  4. mdau hapo juu kwenye budget ya ccm sikuwai kuona wametenga pesa kwa ajili ya kununua meli walizoaidi kwenye kampeni au madaraja au mikopo ya wakulima kama walivyosema kwenye kampeni mwaka jana. jaribu kuwa fair kwenye maoni yako.

    ReplyDelete
  5. Jambo la muhimu hapa ni kutanguliza Utaifa na maslahi ya wananchi, siku zote ushabiki wa kisiasa ukitangulizwa mbele,ari na hamasa binafsi huamka na kuviza fikra sahihi za uwajibikaji, hebu tutangulize Utaifa tuacheni mambo ya siasa katika maendeleo yetu.

    ReplyDelete
  6. siye huyu shibuda mliyekuwa mnamtukana? vijibwa vya Slaa ndio vilivyo hatushangai

    ReplyDelete
  7. Wewe Shibuda acha ujinga ulienguliwa CCM ukakimbilia CHADEMA ni uroho wa fedha tu uluokutuma kugombea tena ubunge.

    ReplyDelete
  8. haya sasa vile vijibwa vya Slaa vimemgeuka tena Shibuda

    ReplyDelete