Na Elizabeth Mayemba
KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia yake Balimi Extra Lager imezindua mashindano ya ngoma za asili kwa mwaka huu, ambayo yanatarajia kuanza kutimua
vumbi Jumamosi katika mikoa mitano ya Kanda ya Ziwa.
Mikoa ambayo mashindano hayo yatafanyika ni Mwanza, Shinyanga, Tabora, Mara na Kagera ambapo fainali zake zitafanyikia Jijini Mwanza Julai 9 mwaka huu.
Akizungumza Dar es Salaam jana Meneja wa bia hiyo Edith Bebwa, alisema Balimi Extra imekuwa mdhamini wa mashindano hayo kwa miaka saba sasa, lengo kubwa likiwa ni kushirikiana na wakazi wa Kanda ya Ziwa katika kuenzi na kulinda tamaduni za kanda hiyo.
"Mashindano ni njia mojawapo kwa wakazi kujipatia kipato cha ziada kupitia zawadi mbalimbali, zitakazotolewa na bia ya Balimi, pia maboresho makubwa yamefanyika kwa mwaka huu, ikilinganishwa na yale ya mwaka jana, na zawadi zimeongezeka mara dufu lengo ni kutoa changamoto kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa," alisema Edith.
Alisema mshindi wa kwanza katika ngazi ya mkoa atajinyakulia kitita cha sh. 500,000, wa pili sh. 400,000, wa tatu sh. 300,000, wa nne sh. 200,000 na mshindi wa tano hadi wa kumi kila kikundi kitapata sh. 100,000.
Edith alisema mshidi wa kwanza katika fainali ataondoka na sh. 1,000,000, wa pili sh. 750,000, wa tatu sh. 500,000, wa nne sh. 400,000 na wa tano hadi kumi kila kikundi sh.300,000.
No comments:
Post a Comment