Na Elizabeth Mayemba
BARAZA la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), limesogeza mbele mashindano ya Kombe la Kagame hadi Julai 25 mwaka huu
ambayo yatafanyikia Dar es Salaam.
Akizungumza kwa njia ya simu jana, Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicholaus Musonye alisema michuano hiyo imesogezwa mbele ili kupata muda wa kutafuta wadhamini.
"Bado tunaendelea kutafuta wadhamini kwa ajili ya kufanikisha mashindano hayo, lengo ni kuyaboresha zaidi," alisema Musonye.
Alisema maandalizi mengine yatafanywa na wenyeji, lakini kwa sasa wanahangaikia wadhamini ili michuano hiyo ianze Julai 25 badala ya Julai 21, mwaka huu kama ilivyopangwa awali.
Musonye alisema Tanzania kupitia viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), bado wapo katika mazungumzo na kampuni mbalimbali kwa ajili ya kupata wadhamini.
Akizungumzia suala hilo, Katibu Mkuu TFF Angetile Osiah, alisema bado wanahaha kutafuta wadhamini ambapo mpaka sasa ni mdhamini mmoja tu aliyejitokeza.
Osiah alisema mdhamini huyo ambaye hakutaka kumtaja jina lake, atagharamia usafiri wa kuzileta timu shiriki nchini na gharama nyingine zitabebwa na wadhamini wengine ambao bado wanawatafuta.
No comments:
Post a Comment