Na Carlos Mtoya
MENEJA wa Shirika la Ugavi Tanzania (Tanesco) Mkoa maalumu wa Ilala Dar es Salaam, Bw. Innocent Luoga amekiri kuwepo kwa malalamiko ya wateja wa
shirika hilo kuhusu usumbufu unaofanywa na wanaojifanya wafanyakazi wa shirika hilo maarufu kama vishoka wakishirikiana na baadhi ya maafisa wa shirika wasio waaminifu kukiuka maadili ya kazi yao.
Akizungumza na Majira ofisini kwake jana, Bw. Luoga alisema hata hivyo usumbufu huo kwa namna nyingine ni wa kujitakia kwa wateja wenyewe kwa kuwa licha ya kufanyiwa vitendo kinyume na sheria bado wamekuwa hawatoi ushirikiano kwa shirika ili kuwanasa vishoka hao.
"Wakati mwingine shirika linatupiwa lawama ambazo kimsingi zinachangiwa na wateja wenyewe kwa sababu wao ndio wanawajua watu wanaofanya hujuma hizo na hawatoi taarifa kwetu ili sisi tuchukue hatua," alisema.
Aliongeza kuwa katika kupambana na hali hiyo shirika liliwahi kutangaza donge nono kwa mwananchi yoyote atakayetoa taarifa kuhusu hujuma dhidi ya shirika na watu wanaojifanya ni wafanyakazi wa TANESCO ambao ndio wamekuwa wakiwatapel. Hata hivyo kasi ya kazi ya kushughulikia tatizo hilo si kubwa kama shirika lilivyotarajia.
Alisema kwa sasa katika mkoa wake wa Ilala kuna timu inayofuatilia watu hao ikiongozwa na afisa usalama wa shirika lakini bado juhudi za kuwatambua wahujumu hao zimekuwa ngumu kutokana na kukosa ushirikiano na wanaotoa malalamiko.
Akielezea kuhusu madai ya wafanyabiashara wa mitaa ya Aggrey na Likoma waliolalamika kuchangishwa fedha na vishoka wanaofika kwa kutumia magari ya shirika, alisema tayari amekwisha weka mtego na hata yeye mwenyewe anatarajia kuwatembelea wafanyabiashara hao ili kuzungumza nao.
"Tunaomba watupatie ushirikiano kila tutakapowatembelea na wasiogope kututajia wahusika ili nasi tuweze kuwaondolea kero hiyo," alisisitiza meneja huyo.
Kwa upande wa madai kuwa mitaa hiyo imekuwa ikikatwa umeme hata wakati usio wa mgao meneja huyo alisema eneo hilo limo kwenye orodha ya maeneo yasiyo muhimu kwa shughuli za kitaifa hivyo ni lazima kila mgao ukitokea yakumbwe na adha hiyo.
Alifafanua kuwa yapo maeneo jijini ambayo kamwe shirika haliwezi kukata umeme hata iweje maeneo hayo ni yale nyeti kitaifa kama Ikulu,hospitali zote za serikali na kwenye eneo lolote ambalo viongozi wa kitaifa wanakuwa na shughuli zao kwa wakati huo.
Hata hivyo, alisema njia za umeme zinazopita kulekea katika maeneo hayo nyeti hunufaisha pia majirani zilipopita njia njia hizo jambo ambalo limekuwa likidhaniwa na baadhi ya watu kuwa shirika linatoa mgao kwa upendeleo wakati ambapo ni kuzingatia majukumu ya kitaifa.
huyu meneja anaposema wateja hawatoi ushirikiano mi sikubaliane nae kwani, mimi mwenyewe mwaka jana nilikwenda kutoa taarifa pale ofisi za kinondoni kuhusu kishoka mmoja maarufu sana pale ubungo, na hawakuwa tayari kunisikiliza! nakushangaa sana bwana wewe!!
ReplyDelete