07 June 2011

Kesi ya uchaguzi Segerea: Fred Mpendazoe aendelea kumng'ang'ania Dkt. Mahanga

Na Rehema Mohamed

MAHAKAMA Kuu imetupilia mbali ombi lililowasilishwa na Mbunge wa Jimbo la Segerea Dkt.Makongoro Mahanga na wakili wa serikali, Bw.David Kawaya, la kutaka
mahakama hiyo ifute kesi ya kupinga matokeo ya ubunge katika jimbo hilo.

Mlalamikaji katika kesi hiyo ni aliyekuwa mgombea ubunge kwa tiketi ya CHADEMA,  Bw.Fred Mpendazoe.

Uamuzi wa mahakama ulitolewa jana mahakamani hapo na Jaji Profesa Ibrahim Juma.

Jaji Juma aliwapa muda wa siku 14  mawakili wa Bw.Mpendazoe kufanyia marekebisho hati ya madai ili kesi hiyo ianze kusikilizwa.

Marekebisho hayo ni pamoja na kuondoa vituo vya kupigia kura ambavyo vilikuwa eneo la Buguruni, Tabata na Kipawa  ambavyo katika hati hiyo, havikutajwa mahali halisi vilipokuwa, ambavyo kasoro yake ilikuwa ni kutohesabiwa kura zake.

Ilielezwa kuwa katika hati ya madai kuna  baadhi ya aya zimefumbwa hivyo itampa shida mlalamikaji katika kuandaa utetezi wake.

Kesi hiyo itajwa Juni 22, mwaka huu tayari kupangiwa tarehe ya kusikilizwa.

Mei 25, mwaka huu wakili wa Dkt.Mahanga ,Bw.Jerome Msemwa na Bw.Kawaya waliwasilisha mahakamani hapo  maombi ya kutaka kufuta kesi hiyo kwa madai kuwa hati ya kesi hiyo ina kasoro za kisheria.

Bw.Mpendazoe katika madai yake anaitaka Mahakama Kuu itengue ushindi wa Dkt. Mahanga kwa kuwa taratibu za Sheria ya Uchaguzi ya Mwaka 2010 hazikufuatwa.

Kabla ya kuahirishwa kwa kesi hiyo, yalitokea mabishano makali ya kisheria, ambapo, wakili wa Bw. Mpendazoe, Peter Kibatala na wa mlalamikiwa (Dkt.Mahanga), Bw.Jerome Msemwa ambaye  aliiomba mahakama kufute shauri hilo.

Alidai kuwa  Bw.Mpendazoe hakufuata taratibu wakati wa kufungua kesi hiyo, ambapo ilitakiwa ianze kusikilizwa kasoro zote za kisheria mbele ya Msajili wa Mahakama Kanda na baada ya hapo ifikishwe kwa jaji.

Alidai kuwa kutokufanya hivyo, kunakiuka kifungu cha 8 kidogo cha (1) cha sheria ya uchaguzi ya mwaka 2010, ambapo jalada linatakiwa kufikishwa kwa msajili ili kusikiliza kasoro za kisheria au makosa mbalimbali ili yafanyiwe  marekebisho kabla ya kufikishwa kwa jaji kusikilizwa.

Pia, wakili huyo alidai kuwa katika hati yake ya malalamiko Bw.Mpendazoe hakutaja majina ya vituo ambavyo anadai vilifanyiwa uchakachuaji wa kura na kwamba hakuna maelezo ya kutosha hivyo mahakama ifute kesi hiyo.

No comments:

Post a Comment