08 June 2011

Taifa Stars kujipima Qatar

Na Zahoro Mlanzi

TIMU ya taifa 'Taifa Stars' inatarajia kujipima na timu za Qatar, Palestina, Shelisheli na Umoja wa nchi za Falme za Kiarabu (UAE) Agosti 10, mwaka huu kabla ya
kuumana na Morocco.

Taifa Stars itacheza na timu mojawapo kati ya hizo katika tarehe hiyo ikiwa ni siku maalumu katika kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), kwa mataifa mbalimbali kucheza michezo ya kirafiki.

Mchezo huo kwa Stars ni kwa ajili ya kujiandaa na mechi ya marudiano dhidi ya Morocco, katika kuwania kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika zitakazofanyika mwakani katika nchi za Guinea ya Ikweta na Gabon.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Angetile Osiah alisema wamepata mialiko kutoka katika mataifa hayo manne yakihitaji kujipima nguvu na Taifa Stars.

"Tumepata mwaliko kutoka Shelisheli wakituhitaji tucheze nao Agosti hapa nyumbani na pia nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu, Qatar na Palestina pia zimeomba lakini hizo zimetutaka tuzifuate nchini mwao," alisema Osiah.

Alisema pamoja na maombi ya nchi hizo, wanamsubiri Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Jan Poulsen kuamua wacheze na timu ipi baada ya kuangalia uzito wa mchezo uliopo mbele yao.

Mbali na kumsubiri Poulsen kuamu hilo, pia atawasilisha ripoti ya mchezo uliopita dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, ambao walifungwa mabao 2-1 ambapo vyote kwa pamoja wataviangalia na kujua nini cha kufanya kabla ya mchezo dhidi ya Morocco.

Kwa mujibu wa viwango vinavyotolewa na FIFA kila mwezi kati ya nchi zilizoomba kujipima na Taifa Stars ni nchi za Qatar na Umoja wa Falme za Kiarab ndizo zilizoizidi Tanzania.

Qatar yenyewe ipo katika nafasi ya 92, UAE ipo nafasi ya 111, Shelisheli ipo nafasi ya 194 na Palestina ambayo miezi kadhaa ilicheza na Taifa Stars na kufungwa bao 1-0 ipo nafasi ya 171 wakati Taifa Stars ipo nafasi ya 117.

No comments:

Post a Comment