Na Zahoro Mlanzi
BAADA ya kufungwa mabao 2-1 na timu ya taifa ya Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR), Kocha Mkuu wa timu ya taifa 'Taifa Stars', Jan Polsen amemlalamikia mwamuzi
aliyechezesha mchezo huo kwamba amechezesha vibaya.
Taifa Stars iliyo katika Kundi D pamoja na timu za Morocco, Algeria na Afrika ya Kati kwa matokeo hayo imejiweka katika mazingira magumu hasa baada ya kundi hilo kuongozwa na Morocco yenye pointi saba sawa na CAR huku Taifa Stars ikiwa nafasi ya tatu kwa pointi nne sawa na Algeria.
Akizungumza kwa simu kutoka jijini Bangui, Afrika ya Kati jana, Ofisa Habari wa shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema timu hiyo itawasili leo saa 5.30 usiku kutokana na jana kukosa ndege ya kuwafikisha Dar es Salaam.
Alisema kwa mujibu wa Poulsen, mchezo ulikuwa mzuri kwa pande zote mbili ila mwamuzi ndiye aliyesababisha mpaka kupoteza mechi hiyo, kwani alikuwa akipendelea upande mmoja.
"Mbali na hilo, pia hata mazingira tulikofikia hayakuwa mazuri na kwamba kipindi cha kwanza tulicheza katika mvua, kitu ambacho kilitupa wakati mgumu lakini kipindi cha pili hali ilikuwa nzuri na ndiyo maana tukapata bao moja," alisema Wambura.
Akizungumzia nafasi ya Tanzania katika kufuzu kwa fainali hizo zitakazopigwa mwakani katika nchi za Guinea ya Ikweta na Gabon, alisema bado ina nafasi kwani inategemea na michezo miwili iliyobaki.
Alisema uzuri ni kwamba mechi zinazofuata katika kundi lao, walioshinda hivi sasa (Morocco na CAR) wanakutana wenyewe hivyo anachoombea timu hizo zitoke sare tu na kufikisha pointi nane.
"Kama itakuwa hivyo na sisi mchezo unaofuata tunacheza na Algeria nyumbani tukishinda tunakuwa na pointi saba, kitu ambacho kitasababisha tuwe na nafasi nzuri ya kufuzu tukishinda na mchezo wa mwisho ugenini," alisema Wambura.
No comments:
Post a Comment