Na Zahoro Mlanzi
BONDIA Daniel Wanyonyi, kutoka Kenya anatarajia kutua nchini Juni 21, mwaka kwa ajili ya kupambana na Francis Cheka katika pambano lisilo la ubingwa litakalofanyika
Juni 25 Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mratibu wa pambano hilo, Clifold Ndimbo alisema maandalizi ya pambano hilo yanaendelea vizuri na kwamba mabondia wote wanaendelea na mazoezi kambini kwao.
Alisema Cheka amepiga kambi nyumbani kwao Morogoro na Wanyonyi, yupo Kenya akiendelea na mazoezi ambapo pambano hilo litakuwa la raundi 10 na taratibu zingine zinaendelea.
"Tunatarajia pambano litakuwa la aina yake kwani mpinzani wa Cheka ana rekodi nzuri tofauti na mabondia aliocheza nao hapo awali, katika mapambano 14, ameshinda 10 kwa KO, mawili sare na kupoteza yaliyobaki, nina amini pambano hilo litakuwa na ushindani sana," alisema Ndimbo.
Alisema wameamua pambano hilo lifanyike mkoani humo kutokana na wakazi na mashabiki wa Cheka, kuomba kwani kila siku wamekuwa wakisafiri nje ya mkoa wao kushuhudia bondia wao akipambana.
Ndimbo alisema Oganaizesheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBO), ndiyo itakayosimamia pambano hilo na kwamba wameshatoa baraka kwa pambano hilo kufanyika.
Naye Rais wa TBPO, Yassin Abdallah 'Ustaadh', alisema licha ya kusimamia pambano hilo wamewapa masharti waandaaji kwamba lazima wahakikishe kunakuwa na ulinzi wa kutosha kwa mtu yeyoto uwanjani kushuhudia pambano hilo.
"Mbali na hilo pia lazima wahakikishe mabondia wote wanapimwa HIV, kwani mchezo huo unaaminika na wataalamu wa afya kwamba ni hatarishi, hivyo ni lazima mabondia wote wapimwe.
Alitolea mfano kwamba huko Ulaya, mabondia wanapimwa HIV zaidi ya mara mbili ndipo wanapanda jukwaani, hivyo ametoa wito kwa mabondia nchini kujijengea mazoea ya kupima HIV.
No comments:
Post a Comment