Na Elizabeth Mayemba
KOCHA Mkuu wa Simba Moses Basena, amemuweka Emmanuel Okwi katika uangalizi wa mechi tatu za michuano ya Kombe la Kagame, baada ya kuboronga kwenye
mechi ya Shirikisho dhidi ya DC Motema Pembe Congo DR, ambayo timu hiyo ya Tanzania ilifungwa mabao 2-0 na kutolewa katika michuano ya Kombe la Shirikisho.
Simba iliondolewa kwenye michuano hiyo wiki iliyopita katika mechi iliyofanyika Kinshasa, Congo ambapo Simba ilikuwa ikihitaji sare ya aina yoyote ili iingie hatua ya makundi baada ya kwenda nchini humo ikiwa na faida ya bao ilililipata katika mechi iliyochezwa Dar es Salaam lakini hata hivyo ikafungwa mabao 2-0 na kuifanya kutolewa kwa jumla ya mabao 2-1.
Habari kutoka ndani ya timu hiyo iliyowasili juzi usiku, zinaeleza kwamba mchezaji huyo alipoteza nafasi nyingi za wazi, hali iliyosababisha wachezaji wenzake kumlaumu mara baada ya mchezo huo kumalizika.
"Kocha Mkuu Basena, amempa mechi tatu za kumwangalia kwani kwa jinsi alivyocheza chini ya kiwango nchini, Congo hakuna aliyefurahishwa, mechi ile ilikuwa tushinde lakini nafasi nyingi alizopata alishindwa kuzitumia," zilieleza habari hizo.
Habari hizo zilieleza kuwa karibu dakika 70 za mchezo, Simba ndiyo ilikuwa inashambulia lakini umaliziaji ndiyo ulikuwa tatizo kubwa ambalo liliigharimu timu hiyo.
Chanzo hicho kimedai kwamba baada ya mchezo huo siku ya kurudi nchini, Okwi alikuwa anataka kwenda kwao Uganda ndipo aje Dar es Salaam lakini kocha wake alimkataza na kumuonya endapo atakwenda yatamkuta yaliyomkuta mwenzake Hilary Echesa.
Kauli hiyo inadaiwa ilimfanya mchezaji huyo aahirishe safari hiyo na kurejea nchini na wenzake kwa ajili ya maandalizi ya michuano ya Kombe la Kagame.
mbazi zikishindwa kuota husingizia mvua....msimuonee mbona wengine hawakufunga magoli..........kama yeye alikuwa anakosa
ReplyDeleteYaani katika timu nzima ya Simba ina maana mshambuliaji alikuwa ni yeye mwenyewe?.Na wengine walikuwa wapi?,Haya ndio matunda ya maandalizi mabovu sasa mnaanza kunyoosheana vidole.Subirini mwakani alafu mrudie uozo uleule.
ReplyDelete