22 June 2011

Yanga 'full nondo' leo Arusha

Na Elizabeth Mayemba

KIKOSI cha timu ya Yanga kikiongozwa na wachezaji wake wa kimataifa Kenneth Asamoah, Yaw Berko na Davies Mwape kinashuka uwanjani leo kucheza na
Gor Mahia ya Kenya mchezo wa kirafiki utakaopigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha.

Yanga inacheza mechi hiyo ikiwa ni kwa ajili ya maandalizi ya michuano ya Kombe la Kagame, inayotarajia kuanza Jumamosi ijayo.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Msemaji wa klabu hiyo, Louis Sendeu alisema kikosi hicho kiliondoka Dar es Salaam jana kwenda Arusha kikiwa kamili.

"Wachezaji wetu wote wamekwenda Arusha kwa ajili ya mchezo huo, ambao ni maalumu kwetu kwa ajili ya kumsaidia kocha Sam Timbe, kupanga kikosi na kufanya marekebisho madogo madogo," alisema Sendeu.

Alisema hata mchezaji wa kimataifa raia wa Ghana, Kenneth Asamoah anatarajiwa kucheza mchezo huo ili kocha naye ajiridhishe na uwezo wake.

Kwa upande wake, Timbe alisema atafanya jitihada za kuwezesha wachezaji wake kuwa katika kiwango kizuri kabla ya michuano ya Kombe la Kagame kuanza.

Alisema ameamua kuanza na programu itakayowezesha wachezaji wake kuwa wepesi na kujua wanachokifanya, wakiwa uwanjani. 

"Nimeona nianze na programu itakayowasaidia kushika yale nitakayowafundisha, tangu wiki iliyopita nimekuwa nikiwapa mazoezi makali ili kuwaweka fiti zaidi na kuwaondolea uchovu wa likizo," alisema Timbe.

No comments:

Post a Comment