*Wafikishwa mahakamani kwa kumjeruhi askari
Na Peter Ringi, Babati
WAFANYAKAZI 13 wa Kampuni ya Ujenzi wa Barabara kutoka China ya (CHICO), jana wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Babati, mkoani
Manyara, kwa tuhuma za kufanya fujo katika Kituo cha Polisi wilayani hapa na kumjeruhi Ofisa wa Polisi Kitengo cha Ulinzi Shirikishi, Bw. Morise Okinda.
Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Bw. Pius Mboko, aliieleza mahakama hiyo kuwa, watuhumiwa hao wenye asili ya kichina, walifanya fujo katika kituo hicho juzi saa 12 jioni.
Alisema kampuni hiyo inajenga barabara kutoka Minjigu hadi Singida ambapo chanzo cha vurugu hizo ni gari la abiria mali ya Kampuni ya NBC, lenye namba T948 AHL, ambalo lilikuwa likitoka Tabora kwenda Arusha, kukwaruza gari la kampuni hiyo baada ya kuteleza kutokana na maji yaliyomwagwa katika barabara wanayojenga Kijiji cha Dudiye.
Aliongeza kuwa, baada ya tukio hilo watuhumiwa walilikamata na kulifikisha kituoni likiwa na abiria, hivyo polisi waliamuru msaidizi wa gari hilo, abaki ili liendelee na safari.
Kitendo hicho kiliamsha hasira za watuhumiwa ambao walilizuia gari hilo na kuanza kuliponda kwa mawe.
Bw. Mboko aliongeza kuwa, askari waliokuwa kituoni walijaribu kuwazuia lakini Mchina mmoja alianza kumshambulia ofisa wa polisi kwa ngumi na mateke.
Wakati mchina huyo akiendelea kumpiga ofisa huyo, wenzake walimzingira ofisa huyo na kuanza kumpiga wakiwa na nondo, bisibisi na kumjeruhi katika paji la uso.
Kutokana na vurugu hizo, askari walianza kujibu mashambulizi kwa kutumia mabomu ya kutoa machozi ili kutuliza ghasia na kumuokoa mwenzao aliyekuwa chini akipata kipigo kutoka kwa Wachina ambao walikuwa na hasira.
Shambulizi la polisi liliwafanya Wachina hao kukimbia ovyo ili kujiokoa lakini walijikuta mikononi mwa wananchi waliokuwa na hasira nao kutokana na manyanyaso wanayofanyiwa wanapofanya kazi zao za ujenzi wa barabara kama vibarua.
Wananchi hao walitumia fursa hiyo kulipiza kisasi kwa kutoa kipigo kikali kilichosababisha Wachina wawili kulazwa Hospitali ya Halmashauri mjini hapa baada ya hali zao kuwa mbaya.
Watuhumiwa hao ni Daogiaa wang (25), Zhani Zu(29), Zuo Jing (41), Jong Jong (26), Guoz Xu (48), Guirgan Xu (43), Liz Wang (29), Jun Lii (38), Yong chea (23), Cheng Wang (25), Pu Chehua (47), Luan Hamfong (23) na Yang Lize (50).
Hata hivyo, Bw. Mboko alimuomba Hakimu Bw. Victor Bigambo, asitoe dhamana kwani upepelezi bado unaendelea na watuhumiwa hawana makazi maalumu, hivyo ni vigumu kuwapata ikiwa watatoroka.
Bw. Bigambo, aliridhia ombi hilo na kuahirisha kesi hiyo hadi Juni 23, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment