*Yataja 18 watakaoivaa Simba
Na Zahoro Mlanzi
WAKATI timu ya DC Motema Pembe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC)ikitarajiwa kutua nchini kesho kwa ajili ya mchezo wao wa
Jumapili dhidi ya Simba, uongozi wa klabu hiyo, umemtupia virago Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mohamed Nabi Nassredine 'Nash' kwa kile kinachodaiwa kushindwa kutimiza matakwa ya uongozi.
Mbali na hilo, timu hiyo imeanika majina ya wachezaji 18 watakaokuja Dar es Salaam kwa ajili ya mchezo wa kuwania kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho la Afrika.
Kwa mujibu wa taarifa za mtandao wa klabu hiyo zilizotoka juzi, zilieleza kwamba kulikuwa na minong'ono ya kuondoka kwa kocha huyo tangu wiki iliyopita lakini kwa sasa wanathibitisha taarifa hizo na hilo wameshalifanya.
"Katika kikao kilichofanyika Jumamosi kati ya uongozi na kocha, pande hizo zilikubaliana kusitisha mkataba.Kutokana na hilo Nash hakusafiri na timu kwenda mjini Goma kumkabidhi majukumu Andy M'Futila Magloire," ilieleza taaria hiyo.
Ilieleza uamuzi huo ulitokana na Nash kutokuwa na hali nzuri kiafya tangu alipowasili nchini humo na inadaiwa kulazimishwa kufanya kazi na makocha wengine wawili akiwemo M'Futila wakati yeye hakutaka.
Taarifa hiyo ilieleza zaidi kwamba mara baada ya Nash kuondoka, Andy M'Futila alikabidhiwa benchi la ufundi mara moja na huo ukiwa ni uamuzi wa Rais wa timu hiyo, Antoine Musanganya.
Inadaiwa kocha huyo (M'Futila) ambaye alikuwa kocha msaidizi katika timu ya V Club ndiye alichangia kwa kiasi kikubwa kuondoka kwa Nash ambapo alimsapoti kwa karibu rais huyo katika maamuzi yake.
Nash ndiye aliyeisaidia kuiweka pazuri timu hiyo tangu akabidhiwe mikoba ya kuinoa ambapo moja ya matokeo mazuri aliyoyapata ni kuzifunga timu za Victor ya Uganda na Haras el-Hodoud katika Kombe la Shirikisho na kuifanya itinge hatua hiyo.
Katika hatua nyingine, timu hiyo imeanika kikosi kitakachokuja kuivaa Simba Jumapili Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambao ni makipa Doumbia Losseny na Matamp Vumi Ley, mabeki ni Ungenda Muselenge, Issam Mpeko, Kabiona Kasongo,
Gladys Bokes na Masombo Lino Lino.
Wachezaji wengine ni Bivalve Nkembi, Ilongo Ngasanya, Mukoko Mayayi Bamenga, Landu Makela, Ndjeka Mukando, Nkanu Mbiyavanga, Bokota Labama, Salakiaku Matondo Salakiaku, Jean-Jacques Yemweni Ngidi, Dama Diavite na Inasawa Mfumu.
Maandalizi ya Simba kwa kweli hayalingani na mchezo ulio mbele yao.Timu wanayocheza nayo mpaka hapo ilipofika imeshaitoa katika mashindano timu ngumu ya Haras el hadoud ya Egypt.Wakati hao Haras el Hadoud walishaitandika Simba bao 5-1 mwaka jana alafu maandalizi yenyewe ni ya kujipima nguvu na timu ya mchanganyiko ya mkoa wa Tanga.Haya tusubiri tuone kitakacho fuata siku ya mchezo.
ReplyDelete