06 June 2011

Madawati ya mbunge kuwaponza madiwani

Na Wilhelim Mulinda, Musoma

MADIWANI watano wa Halmashauri ya Manispaa ya Musoma, mkoani Mara, wanatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa kwa tuhuma za kuvunja
darasa na kuchukua madawati 468 katika Shule ya Msingi Mukendo iliyopo mjini Musoma.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini
hapa, Kamanda wa Polisi mkoani Mara, Bw. Robert Boaz aliwataja watuhumiwa hao kuwa na vyama wanavyotoka vikiwa kwenye mabano kuwa ni Diwani wa Kata ya Kigera, Bw. Gabriel Ocharo (CUF), Diwani wa Kata ya Mwisenge, Bw. Bwire Nyamwero na Bw. Zedi Sondobi ambaye ni Diwani wa Kata ya Bweri.

Wengine ni Bw. Tarai Siza wa Kata ya Kitaji na Bw.
Aloyce Renatus kutoka Kata ya Makoko ambao wote wanatoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Bw. Boaz alisema kuwa madiwani hao wanatuhumiwa kwenda shuleni hapo na kuvunja darasa yalimokuwa yamehifadhiwa madawati hayo mali ya aliyekuwa Mbunge wa Musoma (CCM) Mjini kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana, Bw. Vedastus Mathayo
na kuondoka nayo.

Alisema kuwa hadi sasa polisi imeishawahoji madiwani hao kuhusiana na tuhuma hizo na jalada hilo limepelekwa kwa Ofisi ya Mwendesha Mashtaka kuona kama watuhumiwa hao wana kesi ya kujibu au la.

Pia Kamanda huyo alifafanua kuwa polisi bado wanaendelea na uchunguzi kuona kama madiwani hao walikuwa na sababu ya msingi ya kwenda kuvunja darasa na kuchukua madawati hayo bila kufuata utaratibu uliotumika kuyahifadhi.

“Suala hili linatakiwa kuchungunzwa kwa kina ili kujiridhisha kabla ya kulifikisha mahakamani, kwani pamoja na kuwagusa wanasiasa lakini sheria inabaki pale pale,”
alisema.

Wakizungumza na wandishi wa habari kwa niaba ya Madiwani wenzao, Bw. Sondobi, Bw. Nyamwero pamoja na Bw. Ocharo  walikiri kuchukua madawati hayo shuleni hapo Mei 5, mwaka huu na kudai kuwa walifanya hivyo kwa lengo la kutekeleza majukumu yao kama wawakilishi wa wananchi.

Bw. Mathayo kwa upande wake alisema kuwa dawati moja liligharimu sh. 40, 000 ambapo yeye binafsi alichangia Sh. 30, 000 na kumtaka mwananchi yeyote anayehitaji dawati kwa ajili ya mtoto wake kulipa sh. 10,000 kwa Ofisa Elimu wa Manispaa hiyo ili baadaye fedha hizo zitumike kununulia madawati mengine kukabiliana na upungufu wa madawati mashuleni.

2 comments:

  1. Kama hayo madawati ni mali ya mbunge aliyeshindwa bw. Mathayo kwa nini basi yatunzwe kwenye shule ya serikali? si angeyatafutia ghala ili kila anayenunua anachukua order yake. Mambo ya ajabu kabisa haya, na serikali imekaa kimya inashangilia tu upuuzi huu.

    ReplyDelete
  2. Bado tunashindwa kueleza ukweli. Mbunge huyo aliwahi kutamka kuwa atatengeneza madawati 1000 kwa hela yake iweje akatoa masharti ya mzazi kulipia sh.10000? Na mbaya zaidi kuna fununu kuwa fedha hazikuwa zake ni za mfuko wa jimbo. Hapa wa kueleza ukweli ni afisa Elimu

    ReplyDelete