06 June 2011

Kikwete awashukia viongozi wa dini

Na Kassian Nyandindi, Mbinga

RAIS Jakaya Kikwete amewaonya viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini hapa nchini kuacha tabia ya kushiriki biashara ya kuuza dawa ya kulevya na badala yake
washirikiane na viongozi wa serikali katika kudhibiti biashara hiyo haramu.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Rais Kikwete wakati akihutubia waumini wa dhehebu la Kanisa Katoliki jimbo la Mbinga kwenye ibada maalum ya kupewa daraja la Uaskofu na kusimikwa kwa Mhashamu Askofu John Ndimbo wa jimbo hilo katika kanisa la kiaskofu la mtakatifu Killian.

Ibada hiyo pia ilihudhuriwa na Rais Mstaafu Benjamini Mkapa.

Rais Kikwete alisema kuwa baadhi ya viongozi wa dini wamekuwa wakishiriki biashara ya dawa za kulevya kwa kuwafanya mipango ya kuwatafutia  vijana hati za kusafiria kwenda nchi za nje kufanya biashara hiyo.

Kutokana na hali hiyo aliwataka viongozi wa dini kukemea biashara hiyo na kujenga uhusiano mzuri na vyombo vya dola kuhakikisha biashara hiyo haramu inakomeshwa kwa kuwafichua wahusika wanaofanya biashara hiyo ili wachukuliwe hatua za kisheria.

“Inasikitisha sana na kutisha biashara hii haramu sasa inawavutia hata watumishi wa Mungu, Taifa letu litaharibika tusipokuwa makini katika hili, baadhi yenu tumewakamata”,

“Kauli zenu kemeeni jambo hili kwa kuelimisha jamii hususani vijana waweze kuepuka na matumizi ya dawa ya kulevya,” alisema Rais Kikwete.

Aliyataka madhehebu ya dini hapa nchini katika mipango yake ya kimaendeleo kuwa na mipango endelevu ya maendeleo ya ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi ili kuisaidia jamii katika ushindani wa soko la ajira.

Alifafanua kuwa kutokana na wananchi wengi kukabiliwa na tatizo kubwa la ajira ni vyema sasa serikali kwa kushirikiana na madhehebu ya dini kujikita zaidi katika kujenga vyuo vya ufundi ambavyo vitasaidia kupunguza kero iliyopo ya ukosefu wa ajira hususani vijana wanaomaliza elimu ya msingi na sekondari.

“Kufanikiwa kwa viongozi wa dini katika shughuli za kimaendeleo ni faraja kwa serikali iliyopo madarakani na Watanzania wote kwa ujumla,” alisema.

Kwa upande wake Rais wa Baraza la Maaskofu Kanisa Katoliki Tanzania Askofu Yuda Thadei Ruaichi aliiomba serikali kuhakikisha inazingatie maendeleo ya watanzania katika bajeti inayotarajiwa kupitishwa katika bunge hili.

Pia aliitaka serikali kudumisha amani na utulivu kwa kuhakikisha wakati wote vitendo vya vurugu visipewe nafasi kamwe na kwamba kanisa Katoliki litaendelea kushirikiana na serikali na watanzania wote bila ubaguzi wa rangi, dini au ukabila.

Pamoja na mambo mengine Askofu mpya wa Jimbo la Mbinga John Ndimbo baada ya kusimikwa alitoa shukurani zake kwa Rais Kikwete na waumini wa jimbo hilo kuwa katika uongozi wake atakuwa bega kwa bega kuhakikisha anashirikiana na serikali katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo.

Hata hivyo Askofu Ndimbo alisema kuwa kazi yake kubwa ni ya kuwachunga kondoo wa Mungu pamoja na kuwahamasisha waumini wa jimbo hilo kuwa wanajikita katika kilimo cha kisasa ambacho kitawasaidia kupunguza ukali wa maisha.

4 comments:

  1. Hivi kweli Rais anao ushahidi wa kutosha hadi kushusha tuhuma nzito kama hizi? Ni watu au vijana wangapi wametumwa na taasisi kwenda kuchukua madawa ya kulevya? Halafu madhehebu hao ya dini yayafanyie nini madawa hayo? Halafu madhehebu ya dini ndiyo yanayotoa passport hadi Rais kusema madhehebu hayo yanawatafutia vijana passport? Labda mwandishi umemnukuru vibaya Rais? Kama ni kweli basi Rais wetu amechoka kufikiri jamani. Hizi ni tuhuma kubwa mno kwa kiongozi wa nchi kusema hivyo. Nafikiria kama taasisi za usalama, polisi na taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa zingeshushiwa hivyo tayari serikali ingekuwa imetoa matamko, vitisho na kukamatwa msemaji.

    ReplyDelete
  2. viongozi wa madhehebu ya DINI hawauzi madawa ya kulenvya. Mheshimiwa raisi amekosea na angesema hivi " VIONGOZI WA MADHEHEBU MBALI MBALI YA DINI NISAIDIENI KATIKA SERIKALI YANGU YA CCM KUNA WAUNZA UNGA NA MIMI RAIS WA NCHI NIKIWEMO PAMOJA NA MARAFIKI ZANGU WALIONIWEKA MADARAKANI"

    ReplyDelete
  3. JK tahadhari uwe na uhakika wa kweli kweli kuhusu tuhuma hizi. Isije kuwa "ulimi ulikiponza kichwa". Viongozi wa dini wakiamua kukushukia ili utoe ushahidi thabiti, ni heri ukawa nao, lakini kama ni usanii wako wa maneno kwenye kila jambo, imekula kwako. Mwezi Februari ulisema humjui mmiliki wa Dowans, ghafla juzi juzi unaipigia chapuo inunuliwe na kuwashwa na Wamarekani. Duh Rais wa ajabu kweli wewe! Unasahau mara hii kwamba ulituambia humjui wala hujawahi kumwona mmiliki wake? Au wewe ndiye mwenye akili ya kusahau kama ya mbu anayefukuzwa sikio la kushoto halafu anahamia la kulia kwa kusahau kuwa ni masikio ya mtu mmoja?.

    ReplyDelete
  4. Jamani kunadini nyingi Tanzania(Uyahudi,Uhindu,Ubudha,Uislamu,Ukristu,na dini za jadi) hivyo basi kunaviongozi wengi wa dini kwahiyo wao kama wanadamu wanaweza kufanya jambo lolte kinyume cha maamrisho ya dini zao. Nyie mnaodai ushaidi hamjaona viongozi wa dini wakinywa pombe,wakizini, wakibaka, wakiiba wakisema uwongo hayo yote yana hukumu sawa mbele ya dini zao vipi iwe ajabu kuuza au kula dawa za kulevya Tuanche unafiki.

    ReplyDelete