* Watanzania watarajia kupunguza ukali wa maisha
Na Tumaini Makene
WAKATI Waziri Mustafa Mkullo akitarajiwa kusoma makisio ya matumizi na mapato ya serikali kwa mwaka mpya wa fedha 2011/2012, bungeni leo, Watanzania
watakuwa wakisubiri kwa hamu kujua jinsi ambavyo bajeti hiyo italenga kuwasaidia kupunguza umaskini, ukali wa maisha unaowakabili sasa na kuongeza kipato.
Bajeti hiyo inatarajiwa kuakisi maneno ya Bw. Mkullo ambaye hivi karibuni alinukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari, akisema "Mimi najiandaa kwenda kuwapunguzia wananchi ugumu wa maisha tukienda Dodoma.
Bajeti hiyo inayotarajiwa kufikia trilioni 13- kutoka trilioni 11.7 ya mwaka wa fedha 2010/2011, inatarajiwa kuonesha namna serikali inavyokabiliana na sababu tatu, ambazo kwa mujibu wa Gavana wa Benki Kuu (BoT), Profesa Beno Ndullu, ndiyo chanzo cha ukali na kupanda kwa gharama za maisha.
Kwa mujibu wa Gavana Ndullu akizungumza mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) hivi karibuni, alizitaja sababu za kupanda kwa gharama za maisha kila kukicha kuwa ni; bei ya mafuta, kupanda kwa gharama za umeme na bei ya chakula.
Bei ghali za nishati hasa mafuta na umeme, zinaathiri na kuongeza gharama za uzalishaji na usafirishaji wa bidhaa, huku ukosefu wa chakula kutokana na kuzorota kwa uzalishaji na usafirishaji halikadhalika ni mwiba kwa maisha ya Mtanzania.
Pia bajeti hiyo inatarajiwa kuonesha namna ambavyo Watanzania sasa wataanza kunufaika na takwimu za ukuaji wa uchumi wa Tanzania, ambao umekuwa ukielezwa na wataalamu unakua vizuri kwa wastani wa asilimia 6 takribani miaka 10 iliyopita.
Tegemeo jingine la Watanzania kutoka katika 'mkoba' wa Bw. Mkullo leo bungeni, ni namna Tanzania itakavyoepuka au kupunguza matumizi makubwa katika uendeshaji wa serikali, kuliko inavyoweza kuingiza pato lake, na badala yake sasa fedha nyingi zielekezwe katika miradi ya maendeleo.
Mathalani katika bajeti inayoelekea kuisha mwisho wa Juni, takribani trilioni 7.3 zilitengwa kwa ajili ya matumizi ya serikali, huku sh. trilioni 4.6 pekee ndizo zikitengwa kwa ajili ya uwekezaji katika miradi mbalimbali.
Katika utafiti wake mwaka jana, Taasisi ya Uwazi-Twaweza ilibaini kuwa serikali ilikuwa ikitumia karibu sh. 1.9 huku ikikusanya sh. 1 katika mapato yake, ambapo ilielezwa kuwa tofauti iliyopo inajazwa kwa kukopa fedha na misaada kutoka kwa wafadhili.
Hali hiyo ya matumizi makubwa kuliko kipato na utegemezi mwa nje, umesababisha deni la taifa kuzidi kuongezeka kwa kasi ndani ya mwaka mmoja uliopita, kutoka dola bilioni 9 mpaka dola bilioni 11.
Ongezeko hilo ambalo liliwatisha wabunge katika semina yao mapema Aprili, mwaka huu, ni ongezeko la asilimia 18, ambapo mmoja wa wabunge hao alisema 'kwa hesabu za watu milioni 40, kwa deni hili hata mtoto aliyezaliwa leo anadaiwa dola 245, ilhali hakuhusika kukopa'.
Kuongezeka kwa deni la taifa kuna athari kubwa kwa walipa kodi kwani ndiyo watakaowajibika kulilipa hata kama hawajui lilikopwa kwa sababu gani au bila kujali kama mkopo huo uliwafikia kwa njia ya miradi ya maendeleo au la.
Katika bajeti ya leo pia changamoto nyingine itakayomkabili Bw. Mkullo ni mipango mingi ya serikali kukosa utekelezaji, kutokana na ukosefu wa fedha halisi katika miradi hiyo na kukosekana kwa uwajibikaji wa viongozi katika kuitekeleza.
Wananchi wengi pia wameendelea kuhoji juu ya kushuka kwa thamani ya shilingi, mfumuko wa bei hasa katika bidhaa za vyakula, matumizi ya dola katika manunuzi ya vitu madukani, hotelini.
Ahadi za Rais Jakaya Kikwete, hasa zile za 'papo kwa papo' alizozitoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka jana, ambazo zimeonekana kuwaumiza vichwa wabunge wengi majimboni kwao, zitamwandama Bw. Mkulo, ambaye katika semina ya wabunge alipobanwa, aliahidi kuwa zitaingizwa katika bajeti ya mwaka huu.
Pia kwa mujibu wa wachambuzi wa masuala ya uchumi waliozungumza na Majira juu ya mategemeo yao katika 'mkoba' wa leo wa Bw. Mkulo ni namna ambavyo Tanzania itaepuka au kupunguza utegemezi kutoka kwa wafadhili katika kuchangia mfuko mkuu wa bajeti.
Kwa mujibu wa ripoti mbalimbali za masuala ya uchumi, Tanzania ni ni moja ya nchi 10 duniani ambazo zinaongoza kwa kupokea misaada, lakini imekuwa ikihojiwa mara kwa mara na wachambuzi wa masuala ya uchumi matokeo ya misaada hiyo.
Hivi karibuni akizungumza na vyombo vya habari, Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Fedha Duniani (IMF), Bw. John Wakeman-Linn, aliitaka Tanzania kupunguza kukopa katika kuendesha serikali.
Moja ya maeneo ambayo yamekuwa yakitajwa kuwa yanaweza kusaidia Tanzania kuongeza pato lake la taifa ili kupunguza utegemezi ni kuongeza wigo wa ukusanyaji kodi, mkakati ambao unapaswa uende sambamba na kupunguza misamaha na kuziba mianya ya ukwepaji kodi.
"Watanzania wengi wanatarajia bajeti itakayowapunguzia mzigo wa kodi. Tunategemea katika bajeti hii serikali iongeze tax base (wigo wa kodi), si kutegemea vyanzo vile vile vya mapato...mwendo ule ule miaka nenda miaka rudi...waje na vyanzo vipya sasa," alisema Dkt. Bilame alipozungumza na Majira jana.
"Wananchi wanatarajia serikali itakuja na bajeti yenye mwelekeo wa kutengeneza ajira, kuongeza kipato...wafufue viwanda vya zamani ili watengeneze ajira na kuwapatia kipato wananchi. Katika madini pia wachimbaji wadogo wadogo wapate nafasi ya kuchimba, wapate mapato.
"Wakichimba, wao pamoja na wachimbaji wakubwa wachangie pato la taifa kwa kodi, lakini pia tunatarajia serikali itapunguza kodi katika mafuta, kwani hali sasa imekuwa mbaya, wafikirie vyanzo vipya vya mapato kwa kweli," alisema Dkt. Bilame, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT).
moja ya vyanzo vikubwa vya mapato ni ukusanyaji wa kodi. lakini ninawaswasi kweli kama hili litafanyika kwani viongozi wengi wa serikali wamejiingiza katika biashara na ndiyo wanaoongoza kukwepa kodi nchini. magari makubwa, mabasi na mahoteli mengi yanamilikiwa na viongozi na wastaafu wa serikali. makampuni makubwa yanayokuja kuwekeza nchini yanaletwa na viongozi wa serikali wakiwa wanamiliki wa kiasi kikubwa cha share. sasa iliyobaki ni wafanyakazi wa TRA kuchukua hongo ndogo ndogo na kujitajirisha wenyewe kwa wenyewe. itokee siku moja watanzania tuwatokee tuwaulize wamepata wapi majumba makubwa na magari ya kifahari? tuwapeleke kwenye mahakama ya nguvu ya umma.
ReplyDeletehakuna lolote tanzania ni maneno tu wala hakuna utekelezaji, hakuna serikali iliyochoka kama ya sasa.
ReplyDeleteWatanzania Msijidanye hakuna lolote. Serikali ya Kikwete Imejaa uwizi. Hiyo bajeti itakuwa ya kunufaisha viongozi na siyo wanyonge. JK na Serikali yake wote wamechoka. Kodi inakusanywa kwa wanyonge maskini, wafanyabiashara wakubwa wanakwepa kodi ndo maana wanabali majina ya kampuni zao kila mwaka. We angalia makampuni ya simu majina yanabadika kila siku, au angalia mahoteli majina yanabadilika kila siku hiyo mbinu ya kukwepa kodi.
ReplyDeleteWanyonge msitegemee chochote katika badget labda mpaka JK atakapo maliza muda wake. kwa sasa mateso tu