09 June 2011

Chicharito aitolea nje Real Madrid

LONDON, Uingereza

JAVIER Harnandez 'Chicharito' amekataa ofa kutoka Klabu ya Real Madrid kutokana na utii kwa kocha wake wa Klabu ya Manchester, Alex Ferguson.SunSport juzi
lilisema kuwa Real ilikuwa imejiandaa kutaka kumsaini mshambuliaji kutoka Mexico kwa kutaka kwenda moja kwa moja kwa wamiliki wa Manchester United familia ya Glazer.

Real ilikuwa imewataka kutaja bei yao, lakini Fergie anatumaini kuwa 'Little Pea' Chicharito hatakwenda kokote.

Mchezaji huyo umri wa miaka 23, amekataa kugeuzwa kichwa chake na miamba hiyo ya Hispania.

Alisema: "Nimepata hamasa kubwa baada ya kuwa na msimu mzuri nikiwa na United.

"Kuanzia sasa nitalipa fadhila kwa Sir Alex kwa kunileta Ulaya. Ndoto zangu hazijabadilika.

"Ninataka kutwaa makombe mengi ikiwa ni shukurani kwa timu iliyonifungulia milango."

SunSport pia iliweka wazi kuwa United imepanga kuongeza mshara mara tatu kwa Hernandez, katika mkataba wake ikiwa  ni namna ya kumfanya abakie kwa mshahara wa pauni 75,000.

Hernandez alisajiliwa kwa ada ya pauni milioni 6 kutoka klabu ya Chivas ya Mexico, katika msimu wake wa kwanza amefunga magoli 20.

Kwa sasa yuko na timu yake ya taifa ya Mexico, katika michuano ya kuwania Kombe la ubingwa wa CONCACAF ambapo alifunga mabao matatu katika ushindi wa magoli 5-0 dhidi El Salvador kwenye mechi yao ya kwanza.

Lakini Chicharito alisema: "Mimi si alama au nyota. Soka si mchezo kama gofu lakini ni mchezo wa timu nzima."

Wakati huo huo, klabu ya Man United italazimika kutumia pauni milioni 30, ili kuweza kupata saini ya winga Alexis Sanchez kutoka Udinese.

United ilikuwa na matumaini ya kumpata mchezaji huyo kutoka Chile mwenye umri wa miaka 22, pungufu ya pauni milioni 5, lakini timu ya Udinese haitaki kumuuza kwa bei chee.

Sanchez anapenda kusainiwa na United kuliko Barcelona, kwa kuwa anajua anaweza kwenda kusugua benchi kutokana na kuwepo wachezaji wengi wazuri Nou Camp.

No comments:

Post a Comment