06 June 2011

Kalunde Band yamnyakua Bob Rudala

Mwimbaji mpya wa bendi ya Kalunde, Bob Rudala (kushoto) akiimba kwa hisia pamoja na Deborah Nyangi katika onesho la bendi hiyo lililofanyika mwishoni mwa wiki katika Ukumbi wa Trinity hoteli Oysterbay, Dar es Salaam.

Na Mwandishi Wetu

BENDI ya muziki wa dansi ya Kalunde, imemnyakua mwimbaji mahiri wa In Africa Band, Bob Rudala kwa ajili ya kuiongezea
nguvu safu ya uimbaji.

Nyota huyo aliyewika na In Africa Band tayari ameanza kuwa kivutio katika maonesho ya bendi hiyo yaliyofanyika mwishoni mwa wiki katika kumbi za burudani.

Rudala aliweza kuwapagiwisha vilivyo mashabiki wa dansi waliofika katika maonesho yao yaliyofanyika katika kumbi Trinity hoteli Jumatano, Jovich Pub Kawe Beach Jumamosi na jana Geraffe hoteli.

Akizungumza Dar es Salaam juzi katika Ukumbi wa Jovich Pub kiongozi wa Kalunde, Junior Gringo alisema kwamba wameamua kumchukua Bob Rudala ili kuimarisha safu ya uimbaji.

"Tumeamua kumchukua Bob Rudala ili kuiimarisha bendi yetu kwa kuwa sasa tunataka kuingia katika ushindani wa soko la muziki hapa nchini," alisema Gringo.

Gringo alisema Bob Rudala, kwa kiasi kikubwa atasaidia kutengeneza nyimbo zitakazounda albamu yao ya pili baada ya ile ya awali ya Hilda ambayo nyimbo zake zinatamba katika vituo mbalimbali vya redio nchini.

Alisema tayari nyimbo tatu zitakazounda albamu mpya zimeshakamilika ambazo ni Funguo, Cisee na Masumbuko ambazo kwa sasa zimeanza kupigwa katika kumbi mbalimbali wanazopiga.

No comments:

Post a Comment