06 June 2011

Eto'o azamisha jahazi la Cameroon kufuzu CHAN 2012

YAOUNDE, Cameroon

PENALTI ya dakika za mwisho iliyokoswa na mchezaji wa kimataifa, Samuel Eto’o imeifanya Cameroon kubaki na matumaini madogo ya kufuzu fainali za
Mataifa ya Afrika 2012, baada ya kukubali kwenda suluhu na Senegal ikiwa kwenye uwanja wake wa nyumbani mjini Yaounde.

Mkwaju huo wa dakika za mwisho uliopigwa na nahodha huyo wa Cameroon, uligonga mwamba wa juu wa goli, hivyo kuwanyima mabingwa hao mara nne Afrika kuondoka na ushindi katika kampeni zake za kufuzu tena michuano hiyo.

Kwa matokeo hayo Cameroon imebaki nyuma kwa pointi tano dhidi ya vinara wa kundi hilo E, Senegal na imebaki na takribani mechi mbili za kucheza huku ikiwa imeshinda mechi moja kati ya mechi nne, ambazo imeshacheza kufuzu fainali hizo.

Matokeo hayo yaliwafanya mashabiki kuja juu wakiishutumu timu hiyo, hali ambayo iliwalazimu polisi kuingilia kati kwa kutumia maji ya kuwasha ili kuwatawanya mashabiki waliokuwa wakifanya vurugu nje ya Uwanja wa Ahmadou Ahidjo kwa kuzuia basi lililokuwa limebeba wachezaji huku wakimshutumu zaidi Eto'o.

Katika mchezo huo, Cameroon ilijitahidi kwa kila hali kufanya mashambulizi, lakini kipa wa Senegal, Bouna Coulibaly ndiye aliyekuwa kikwazo zaidi kabla ya Eto’o, kukosa penalti hiyo ambayo inaelekea kukifanya kigogo hicho cha soka kuikosa michuano hiyo mikubwa Afrika kwa mara ya pili atika kipindi cha miaka 30.

“Tulikuwa na bahati mbaya,” alisema kiungo wa timu hiyo, Stephane Mbia.

Matokeo hayo pia yanaifanya Cameroon sasa kuhitaji kushinda mechi zake mbili zilizobaki, dhidi ya Mauritius na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) ili iweze kupata nafasi ya kufuzu moja kwa moja, huku yakiwa yamezima pia ndoto za kuwa kati ya timu mbili bora zitakazoshika nafasi ya pili katika makundi 11 ya timu zinazowania kufuzu fainali hizo.

Wakati hali ikiwa mbaya kwa Cameroon, mambo yalikuwa safi kwa timu za taifa za Uganda na Burkina Faso kwa kukaribia kufuzu fainali hizo za mwakani, baada ya kuibuka na ushindi dhidi ya wapinzani wao.

Katika mechi hizo zilizopigwa Juzi, Uganda iliibuka mbabe dhidi ya Guinea-Bissau kwa kuilaza kwa mabao 2-0, matokeo ambayo yanaifanya timu hiyo kukaribia kutinga fainali hizo, ikiwa ni mara ya kwanza tangu mwaka 1978, ilipofungwa hatua ya fainali huku Burkina Faso ikiwa imejisafishia njia ya kwenda katika mashindano hayo yatakayofanyika nchini Gabon na Equatorial Guinea, baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 4-1 dhidi ya Namibia.

Matokeo ya mechi nyingine yalikuwa kama ifuatavyo, Morocco iliwalaza wapinzani wao katika ukanda wa Afrika Kaskazini, Algeria kwa mabao 4-0 katika mechi za kundi D.

Zambia ikaichapa Msumbiji 3-0 na Sierra Leone ikaichabanga Niger bao 1-0 lililoifanya irejee tena katika mbio za kuwania fainali hizo kupitia kundi hilo G lenye timu ngumu za Afrika Kusini na Misri.

No comments:

Post a Comment