01 July 2011

Diwani aishukia Manispaa kwa uzembe

Na Anneth Kagenda

DIWANI wa Kata ya Upanga Magharibi Wilaya ya Ilala Dar es Salaam Bw. Godwin Mmbaga, (CCM) amesema uzembe wa uongozi wa Manispaa hiyo ndio kiini cha
wananchi kuchakachua maeneo na kujenga kiholela.

Akizungumza katika mkutano wa kujadili elimu ya watu wazima na kutoa hamasa kwa jamii kujiunga na elimu hiyo jana, Diwani huyo alisema Manispaa ya Ilala imeshindwa kulinda maeneo ya wazi hiyo kuwafanya wananchi kuyavamia.

Alitaja mfano wa eneo la Jangwani Minazini ambapo watu wamejenga lakini ilitakiwa kuwa eneo la umma kwa ajili ya kituo cha elimu ya watu wazima,shule za chekechea na vyuo.

"Lazima tufike mahali tuseme ukweli, tunajadiliana kuhusu sehemu ambazo watu watakuwa wanapata elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi.

Tunajadili tuweke shelfu za vitabu maktaba kwenye ofisi za Kata lakini ikumbukwe kwamba yapo maeneo ambayo kama Manispaa ingeyasimamia vyema vingejengwa vyumba vya kufundishia watu hao, chekechea, Ofisi za Kata na mambo mengine ya maendeleo," alisema Bw. Mmbaga.

Alisema ardhi ya Kata yake tayari imechakachuliwa hivyo kumpa kigugumizi ya jinsi ya kutekeleza lengo la kujenga kituo cha elimu ya watu wazima.

Kwa upande wake Mratibu wa Elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi Mkoa wa Dar es Salaam, Bi. Benadetha Tomas, alisisitiza umuhimu wa jamii kulewa mfumo huo wa elimu.

Alisema baadhi ya watanzania hawajui kwamba elimu hiyo bado inatolewa hivyo kuongeza kiwango cha watu wasiojua kusoma na kuandika na wale wanaotaka kujiendeleza zaidi kukosa fursa hiyo.

"Ili kuhakikisha suala hilo linafikia malengo jamii inatakiwa kuwasiliana na watoa huduma maeneo yote walipo katika vituo vinavyotoa elimu," alisema.

Alitaja changamoto nyingine kuwa ni  jamii kutoelewa program za elimu hiyo inayotakiwa kusaidia kuinua kiwango cha elimu na kufuta ujinga nchini.

No comments:

Post a Comment