28 June 2011

Ocean View yajiweka pazuri Kagame

Na Elizabeth Mayemba

TIMU ya soka ya Zanzibar Ocean View, imejiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele kwenye michuano ya Kagame Castle Cup, baada ya kuilaza Red Sea ya
Eritrea mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Zanzibar Ocean View walianza mchezo kwa kasi na kulifikia lango la wapinzani wao mapema, lakini washambuliaji wake, hawakuwa makini kukwamisha mpira wavuni.

Dakika ya 36, Ocean View walirekebisha makosa yao na kufanikiwa kupata bao la kwanza lililofungwa na Suleiman Haji, baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Mohammed Hamduni.

Baada ya kupata bao hilo, Ocean View walizidisha mashambulizi, lakini dakika ya 65, Said Rashid alishindwa kutumia vizuri nafasi aliyopata kwa kupiga shuti lililopanguliwa na kipa wa Red Sea, Daniel Goitom.

Bao la pili la Ocean View lilifungwa kwa shuti kali na Said Rashid katika dakika ya 85, aliyeingia kuchukua nafasi ya Amour Suleiman.

Mchezaji Aron Zakarias wa Red Sea alioneshwa kadi nyekundu baada ya kumpiga kiwiko Salum Shebe wa Ocean View

Katika mechi nyingine iliyochezwa uwanjani hapo, timu ya Vital'O ya Burundi iliibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Etincelles ya Rwanda.

Katika mechi yake ya kwanza ya mwishoni mwa wiki, timu hiyo ilitoka suluhu na Simba, hivyo imejikusanyia pointi nne katika Kundi A, ikiwa nyuma ya Ocean View inayoongoza kundi hilo ikiwa na pointi sita.

Bao la kwanza la Vital'O lilifungwa na Nzigamasabo Steve dakika ya sita, baada ya kutumia vizuri nafasi aliyopata na kuukwamisha mpira wavuni.

Dakika ya 61, Etincelles walisawazisha bao hilo kupitia kwa Ochaya Sylvan, kabla ya furaha yao haijamalizika, Etincelles walijikuta wakipachikwa bao la pili lililofungwa na Minzi Stanley.

Dakika ya 66, Vita'O walipata pigo baada ya mchezaji wao, Muhinze Claver kumpiga kichwa Ngabonzima Muhamudu wa Etincelles na mwamuzi wa mchezo huo kuamuru ipigwe penalti.

Hata hivyo, Muhamudu aliikosesha timu yake bao, baada ya kushindwa kufunga mkwaju wa penalti.

Bao la tatu la Vital'O lilifungwa na Mbakiye Baby Miami kwa mkwaju wa adhabu, baada ya mchezaji wa Etincelles  kumchezea vibaya Steve.

Leo, katika mfululizo wa michuano hiyo, Bunamwaya wa Uganda itaumana na Elman ya Somalia, mechi ambayo ni ya Kundi B, wakati St George ya Ethiopia itacheza na Ulinzi ya Kenya ambazo za Kundi C zitakutana kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.

No comments:

Post a Comment