24 May 2011

Yanga yahadharisha wachezaji wake

Na Elizabeth Mayemba

UONGOZI wa Yanga, umetoa hadhari kwa wachezaji wake ambao wana mikataba nao, kufanya mazungumzo na klabu nyingine bila kufuata taratibu, vinginevyo
watachukuliwa hatua za kinidhamu.

Hatua hiyo ya Yanga, imekuja baada ya wiki iliyopita baadhi ya vyombo habari kuripoti kwamba beki wake wa kutumainiwa, Nadir Haroub 'Cannavaro' kutaka kusaini mkataba na Simba kwa ajili ya kuichezea msimu ujao wa Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa.

Akizungumza Dar es Salaam jana Msemaji wa klabu ya hiyo, Louis Sendeu alisema wachezaji wote wanapaswa kupitia vizuri kanuni za mikataba yao ili wasiwe wanakurupuka na kufanya mazungumzo na klabu nyingine.

"Tunatoa hadhari kwa wachezaji wetu wenye mikataba, ikitokea mchezaji anafanya mazungumzo na klabu nyingine tutamchukulia hatua kali za kinidhamu, pia tunawakumbusha wachezaji wetu wajenge utaratibu wa kupitia mikataba yao, ili wasikurupuke kwenye suala zima la usajili," alisema Sendeu.

Alisema bado wamegundua kwamba kuna klabu ambazo zinawanyatia wachezaji wao, hivyo wanatoa onyo kwa klabu yoyote itakayofanya hivyo bila kufuata taratibu zinazotakiwa.

Sendeu alisema hadi kufikia Juni 21, mwaka huu wachezaji wote wapya watasainishwa mikataba mipya kwa ajili ya kuanza rasmi maandalizi ya Ligi Kuu Tanzania Bara, inayotarajiwa kuanza Agosti mwaka huu.

No comments:

Post a Comment