Na Benjamin Masese
SERIKALI kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imetoa jumla ya tani 29,220 za mahindi yenye thamani ya sh. 10,227,000,000 kati ya Septemba 2010 na Mei katika
awamu mbili tofauti katika wilaya 28 za mikoa 12 iliyobainika kuwa na upungufu wa chakula kwa kipindi hicho.
Mbali na hilo imetoa ufafanuzi juu ya hatua ilizochukua kukabiliana na maafa ya mafuriko na upepo ulitokea katika wilaya sita kuanzia mwishoni mwa mwaka jana hadi mwaka huu ambapo jumla ya sh. 1,164,817,000 zilitumika.
Taarifa iliyotolewa kwenye vyombo vya habari Dar es Salaam na Waziri wa Nchi, Sera na Uratibu wa Bunge, Bw. Wiliam Lukuvi na kusema kwamba kulingana na tathimini iliyofanywa na serikali ilibaini wananchi wa wilaya hizo wanakabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula kutokana na sababu mbalimbali ambapo awamu ya kwanza ilitoa tani 13,760 na ya pili tani 15,460 na kupunguza tatizo.
Bw. Lukuvi alizitaja wilaya zilizopewa mahindi kwa awamu ya kwanza ni pamoja na Longido, Monduli, Ngorogoro (Arusha), Bahi, Chamwino, Mpwapwa, Kongwa, Dodoma mjini (Dodoma), Mwanga, Same (Kilimanjaro), Lindi Vijijini, Ruangwa na Liwale (Lindi).
Nyingine ni Babati, Simanjiro,Kiteto (Manyara), Morogoro Vijijini, Mvomero (Morogoro), Nanyumbu na Masasi (Mtwara), Shinyaga Vijijini na mjini, Kishapu, Meatu (Shinyanga), Manyoni mkoni Singida na Kwimba (Mwanza).
Bw. Lukuvi alisema kuwa mbali ya baadhi ya wilaya kupewa chakula kwa awamu ya kwanza bado tatizo liliendelea kuwepo na kulazimika kutoa kwa awamu ya pili.
Alisema wilaya zilizoendelea kukumbwa na njaa na kupewa kwa awamu ya pili ni Shinyanga mjini na vijijini,Bahi, Chamwino, Mpwapwa, Ruangwa, Liwale, Dodoma mjini, Lindi vijijini, Ruangwa na Manyoni.
Bw. Lukuvi alizitaja wilaya zilizopewa kwa awamu ya pili ni pamoja na Bariadi, Rombo, Bukombe, Kahama, Maswa, Kishapu, Iringa vijijini na Nzega.
Aidha alisema kuwa serikali imepokea maombi mapya ya msaada wa chakula kutoka Halmashauri ya Ludewa na mji wa Babati huku Ludewa ikiwa imepelekewa tani 34 na Babati tani 1,000 za mahindi.
Vile vile alisema kuwa serikali inakamilisha taarifa za kina juu ya hali ya chakula katika mikoa saba ambayo inaonekana imeathirika zaidi ikiwa ni pamoja na Lindi, Tanga, Dodoma, Tabora, Iringa, Kilimanjaro na Singida ili kupewa msaada huo.
Bw. Lukuvi alizitaj wilaya sita zilizoathirika na upepo na mvua ni Manispaa ya Songea, Muleba, Musoma, Mvomero, Kilombero na Hanang ambazo zilipata uharibifu mbalimbali ikiwemo miundombinu na kusababisha jamii iliyoathirika kushindwa kujikimu hali iliyohitaji msaada wa kibinadamu.
Bw. Lukuvi aliainisha kiwango cha fedha kilichotolewa kwa kila wilaya ambapo Manispaa ya Songea sh. 37,487,000, Muleba sh.30,965,000, Njombe sh. 2,900,000 na Hanang sh. 76,735,000.
Vile vile alisema Wilaya ya Kilombero serikali ilitoa sh.756,442,000 kugharamia matengenezo ya barabara na madaraja sita yalibomoka pamoja na mahitaji muhimu ya kibinadamu kama mahindi, mafuta ya kupikia, maharage, sukari na chumvi.
Bw. Lukuvi alisema katika Wilaya ya Mvemero serikali ilitoa tani 65 za mahindi na sh. 4,940,000 za usafirishaji kwa ajili ya kuwasaidia wananchi 300 waliothirika ambapo wilaya ya Muleba ilipewa tani 2,076 za mahindi kwa waathirika wa mvua na upepo mkali na sh. 255,348,000 zilitumika kuyasafirisha.
No comments:
Post a Comment