23 May 2011

Simba yaomba mashabiki Cairo

*Wydad kwenda na mashabiki 3,000

Na Zahoro Mlanzi

KLABU ya Simba imetoa fursa kwa mashabiki wake kwenda kuishangilia timu hiyo jijini Cairo, Misri wakati itakapoumana na Wydad Casablaca ya Morocco katika
mchezo wa mashindano ya Klabu Bingwa Afrika kwa kuchangia dola 1,000.

Mbali na hilo, klabu hiyo pia imesema itawagharamia malazi, chakula na upatikanaji wa viza mashabiki hao ili ihakikishe inatinga hatua ya makundi ya mashindano hayo.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ismail Rage alisema lengo lao ni kufika mbali katika mashindano hayo na ndiyo maana wanafanya maandalizi ya nguvu.

"Maandalizi yanaendelea vizuri huko visiwani Zanzibar, ila tunatoa wito kwa mashabiki wetu wanaotaka kwenda kuipa sapoti timu yao huko Misri kutoa dola 1,000, alafu sisi tutawagharamia huduma zingine," alisema Rage.

Alisema malipo yote yawasilishwe kwa Katibu Mkuu, Evodius Mtawala kabla ya kesho ili wapate muda wa kushughulikia viza pamoja na mambo mengine.

Timu hizo zinatarajiwa kuumana Jumamosi katika Uwanja wa Petrosorts Jijini Cairo ukiwa ni mchezo wa kuwania kucheza hatua ya makundi ya mashindano ya Klabu Bingwa Afrika.

Wakati huo huo, wapinzani wao nao, wamesema itawakodia ndege mashabiki 3,000 kwenda nao Cairo, kuishangilia timu hiyo wakati itakapoumana na Simba. 

Kwa mujibu wa taarifa za mtandao wa klabu hiyo, zilieleza jana kwamba kila shabiki atalazimika kuchangia zaidi ya sh. 550,000 ili kwenda kuipa sapoti timu hiyo kwa kuishangilia na hatimaye ifanye vizuri katika mchezo huo.

"Klabu imefungua milango kwa mashabiki wote na wadau wa soka nchini Morocco, kwenda kuipa sapoti timu yao ambapo fedha hizo zitatumika kwa ajili ya usafiri wa ndege kutoka Casablanca mpaka Cairo.

"Pia fedha hizo zitatumika kwa usafiri wa kutoka uwanja wa ndege mpaka katika uwanja ambao mchezo utapigwa, kiingilio cha uwanjani na gharama ya viza," ilieleza taarifa hiyo.

Ilieleza kuwa safari hiyo imepangwa kufanyika Ijumaa na watarudi Jumamosi, baada ya kufanya mkutano ambapo malipo yatapokelewa na Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Haj Mohamed.

No comments:

Post a Comment