Na Mwandishi Wetu
MASHINDANO YA Str8 Muzik Freestyle 2011, yaliyohusisha mikoa mitatu yamefikia tamati huku, Omari Mohamed akitangazwa DJ bora wa Mkoa wa
Dar es Salaam katika tukio lililofanyika katika Ukumbi wa Club Bilicanas, Dar es Salaam.
Katika kinyang'anyiro hicho, Daud Nisan alitangazwa kuwa MC bora katika Mkoa wa Dar es Salaam huku kundi la dansi la Blue Sexy likijinyakulia kitita cha sh. 700,000 kwa kuibuka kundi bora la dansi wakati wa mashindano hayo.
Kwa upande wa mpambano wa ma-DJ, Mohammed aliibuka na ushindi kwa kumbwaga wajina wake, DJ Omari Said aliyeshika nafasi ya pili baada ya kuingia fainali kwenye mchuano huo.
Kutokana na ushindi huo, DJ Mohamed alizawadiwa tuzo maalumu ya Str8 Muzik, mfuko wenye zawadi kem kem na mixer ya kisasa ya muziki.
Kwa upande wake Nisan, aliyetangazwa MC bora alikabidhiwa tuzo Maalumu ya Str8 Muzik, mfuko wenye zawadi na kupewa udhamini wa kurekodi muziki wake katika studio yoyote nchini.
Zawadi zote na tuzo zilikabidhiwa na Ofisa Masoko wa chapa ya Sweet Menthol, Isamba Kasaka.
Mbali na burudani kutoka kwa washindani, zilikuwepo pia burudani kutoka kwa wasanii wa muziki wa kizazi kipya ambao ni TID, Fid Q na Bagdad wakiongozwa na Mexilana Lacavela wa Sinza.
Mashindano haya pia yalifanyika katika Mkoa wa Mbeya na Mwanza hapo awali na kila mkoa kutoa DJ na MC bora.
No comments:
Post a Comment