*Yamteua kamati ya kuchangia usajili
Na Elizabeth Mayemba
MWENYEKITI wa Yanga, Lloyd Nchunga amemwangukia aliyekuwa Makamu wake Davis Mosha, aliyejiuzulu wadhifa huo, na kumteua kuwa mmoja wa
Wajumbe wa Kamati ya Kuchangia fedha za usajili wa wachezaji wapya watakaosajiliwa kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya kimataifa.
Kwa mujibu wa barua hiyo iliyoandikwa na Mwenyekiti wa klabu hiyo Mei 23, mwaka huu, zoezi hilo la uchangiaji wa fedha za usajili linatarajiwa kufanyika Jumapili, kwenye hoteli ya Ragency, Dar es Salaam kuanzia saa 12 jioni.
Katika barua hiyo, Nchunga alimwomba Mosha kuwa mmoja wa Wajumbe wa kamati hiyo, ili kukamilisha zoezi la usajili linalohitaji fedha nyingi.
"Kufuatia zoezi la usajili lililoanza hivi karibuni, uongozi wa klabu ya Yanga umekuteuwa kuwa mmoja wa wajumbe wa kamati ya kuchangia fedha za usajili," ilisema sehemu ya barua hiyo iliyosainiwa na Mwenyekti huyo.
Mwishoni wa msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Mosha aliandika barua ya kujiudhuru wadhifa wake, kwa madai ya kudhalilishwa na kutishiwa maisha na baadhi ya wanachama wa klabu hiyo.
Hata hivyo, kundi kubwa la wanachama wa klabu hiyo walivamia nyumbani kwa Mosha na kumrejesha Yanga, lakini Mwenyekiti wake Nchunga alikataa kumtambua tena makamu huyo kwa kile alichodai kwamba, asubiri Mkutano Mkuu wa Wanachama ambao utaamua hatma yake.
Katika suala la usajili, tayari klabu hiyo imefanya mazungumzo na wachezaji mbalimbali wa kimataifa na wa ndani, hivyo wanamsubiri kocha wao Sam Timbe, ili awaridhie.
Wachezaji wa nje ambao Yanga inadaiwa kutaka kuwasajili ni beki Tonny Ndolo wa Uganda, kiungo Haruna Niyonzima 'Fabregas' wa APR ya Rwanda na mshambuliaji Kenneth Asamoah wa Ghana, ambao wataungana na wenzao wa kigeni Mzambia Davise Mwape na Mghana Yaw Berko.
Wachezaji wapya wa ndani ambao tayari imefanya nao mazungumzo ni kipa wa Majimaji, Saidi Mohammed, kipa wa Mtibwa Sugar na Taifa Stars, Shaaban Hassan 'Kado', mabeki David Luhembe na Godfrey Taita wa Kagera Sugar, Oscar Joshua wa Moro United, kiungo Julias Mrope wa Mtibwa Sugar na Mshambuliaji Pius Kisambale wa JKT Ruvu.
No comments:
Post a Comment