Na Mwandishi Wetu, Mwanza
HOTELI ya kitalii ya Gold Crest ya jijini hapa, imejitokeza kudhamini mashindano ya Miss Mwanza 2011 yanayotarajiwa kufanyika Juni mwaka huu.Akizungumza na
waandishi wa habari jijini hapa juzi msimamizi wa hoteli hiyo,
Benny Mwangi alisema hoteli hiyo imeamua kudhamini mashindano hayo kutokana
na umuhimu wake ndani na nje ya mipaka ya Jiji la Mwanza.
Mwangi alisema kuwa mashindano hayo yatasaidia kukuza sekta ya utalii Jijini Mwanza na hapa nchini kwa ujumla na pia kuwawezesha wasichana watakaoshiriki kupata ajira kwa ajili ya kuendeshea maisha yao.
“Tunaamini mchango unaoletwa na waandaaji wa Miss Tanzania, kwani unaitangaza nchi vizuri, licha ya nchi yetu kutowahi kutwaa taji la Dunia, ‘Miss World’," alisema.
Kwa upande wake, Mratibu wa mashindano hayo, John Dotto, alisema warembo
watakaoshiriki wanatarajia kuingia kambini kuanzia Juni 10 mwaka huu, ambao wataendelea na maandalizi ya fainali itakayokuwa na msisimko wa aina yake.
Aliwataka warembo wenye sifa za kushiriki shindano hilo waendelee kujitokeza
ambapo fomu zinatolewa katika hoteli hiyo ya Gold Crest.
Dotto aliwataja wadhamini wengine kuwa ni Vodacom, Redd’s, PSI, Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) na Fransac General Suppliers.
No comments:
Post a Comment