Na Rashid Mkwinda, Mbeya
SERIKALI imempa wiki mbili Wakala wa Barabara (TanRoads) kutoa maelezo juu ya mkataba wa ujenzi wa barabara ya Singida hadi Nzega ambayo imebomoka ndani ya
miaka miwili baada ya kukamilika.
Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Dkt. Harrison Mwakyembe alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Mbeya baada ya kukamilisha ziara yake ya kukagua barabara maeneo mbalimbali nchini.
"Tupate taarifa za kiufundi ndani ya wiki mbili, kuna kipande cha km 5 barabara ya Singida hadi Nzega imekamilika, ndani ya miaka miwili imebomoka, matarajio yetu ni kuona barabara zinadumu kwa miaka 15 hadi 20," alisema Dkt. Mwakyembe.
Alisema kuwa yeyote atakayebainika kuhusika na hasara hiyo atawajibika iwe kampuni au watendaji wa ndani ya serikali, "Tuitane tuwajibishane, tunamtaka mtendaji wa TANROAD awasilishe taarifa," alisisitiza.
Aidha aliyataka makampuni ya ujenzi wa barabara ya hapa nchini kujitokeza kuchukua zabuni za ujenzi wa barabara kutokana na makampuni mengi ya kigeni kutofanya vizuri.
Alisema kuwa ameridhishwa na ujenzi wa kampuni za kizalendo na kuwa makampuni mengi ya kigeni yaliyokabidhiwa kazi ya ujenzi wa barabara nchini yamekuwa yakifanya vibaya na barabara walizotengeneza hubomoka muda mfupi baada ya kuzikabidhi serikalini.
Dkt. Mwakyembe alisema kuwa amekagua barabara nyingi nchini ambazo zimejengwa na wahandisi wa kigeni zikiwa katika hali mbaya, nyingi zikiwa zimebomoka ilhali zile zilizojengwa na kampuni za kizalendo zikiwa bado katika hali nzuri.
"Tumeridhishwa na ujenzi wa kampuni za Kitanzania…zinazofanya vizuri tuzipe kipaumbele," alisema Dkt. Mwakyembe.
Kadhalika alisema kuwa serikali inatarajia kukamilisha barabara yenye urefu wa kilomita 259.8 kati ya Dodoma na Iringa kwa kiwango cha lami ambayo itagharimu kiasi cha sh. milioni 222.26 na ile ya Nzega-Tabora yenye urefu wa kilomita 1,150 itakayogharimu bilioni 129 na Tabora-Urambo yenye urefu wa kilomita 94 itakayogharimu bilioni 111.
Alisema barabara za Tabora-Nyaihuwa-Urambo-Kariua-Malagalasi serikali inatafuta fedha ili kuzikamilisha ilhali ile barabara ya Mbeya Lwanjiro ambayo awali ilisimama, amekabidhiwa mkadarasi mwingine kampuni ya Chines Construction Company(CCC) kwa gharama ya sh. bilioni 55.
No comments:
Post a Comment