16 May 2011

Simba yapata hasara ya mil. 380

*Kuwarejesha Samatta, Ochan

Na Zahoro Mlanzi

KLABU ya Simba imepata hasara ya sh. milioni 381,393,000, katika msimu wa Ligi Kuu Bara uliomalizika Aprili mwaka huu.Hasara hiyo ilielezwa jana na
uongozi wa klabu hiyo katika Mkutano Mkuu wa mwaka uliofanyika Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wanachama zaidi ya 710, ambao walionekana kuridhishwa na ripoti ya mapato na matumizi.

Pia uongozi huo ulieleza kuwa ipo katika mpango wa kuwarudisha wachezaji wake wawili Mbwana Samatta na Patrick Ochan, waliouzwa kwa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), ili waje kuisaidia timu hiyo katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika.

Akizungumza wakati mkutano huo ukiendelea Dar es Salaam jana, Mkaguzi wa Kampuni ya Audits International, Venance Kisare alisoma ripoti ya mapato na matumizi tangu Desemba 31, mwaka jana na namna walivyotumia fedha hizo.

"Klabu ina vyanzo mbalimbali vya kujipatia fedha, kutokana na vyanzo hivyo kama mapato ya milangoni ya mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara na mechi zingine, ada za wanachama na udhamini wa TBL (Kampuni ya Bia Tanzania), tulitarajia kupata sh. 1, 087,998,000.

"Sasa kutokana na matarajio hayo ya fedha, klabu ikatumia sh. 1, 089,391,000 ambapo ikiangaliwa ni zaidi ya tulichotarajia, hivyo klabu imepata hasara ya sh. 381,393,000 lakini pamoja na hayo tulipata misaada kutoka sehemu mbalimbali iliyofikia sh. 1,469,391,000," alisema.

Aliongeza pamoja na hayo, pia walipata sh. 678,356,478 kutoka katika mambo yao mengine mbalimbali ambapo sh. 666,238,567 walizitumia kwa shughuli zingine na sh. 12,117,919 ndizo zilizopo benki kwa sasa.

Baada ya kumaliza kusoma ripoti hiyo, Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ismail Rage ambaye ndiye aliyefungua mkutano huo, aliwauliza wanachama wake kama wameridhika na mchanganuo wa mapato na matumizi, wote kwa pamoja walionesha kuridhika na mkutano ukaendelea na ajenda zingine.

Rage baada ya hapo, alimtambulisha rasmi Kocha Mkuu mpya wa timu hiyo, Mosses Basena kwa wanachama wao ambapo alipokelewa kwa shangwe na nderemo na kufanya mkutano huo kuwa wa aina yake.

Muda mchache baada ya kutambulishwa, Basena alizungumza mbele ya wanachama kwa kuwashukuru viongozi wa Simba na kuahidi kukisuka kikosi upya, ambapo anatarajia kuwemo katika historia mpya itakayowekwa na timu hiyo.

Alisema anaomba ushirikiano kutoka kwa wanachama na kwamba sasa ameandaa programu ya dharura kwa ajili ya kuikabili, Experance ya Misri katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika baada ya TP Mazembe, kuondolewa kwa kufanya udanganyifu.

Naye Rage aliongeza kuwa, licha ya kuwauza Samatta na Ochan, watazungumza na TP Mazembe waje kuwasaidia katika kampeni zao za kucheza fainali za Klabu Bingwa Afrika kutokana na wachezaji hao kuwa na leseni ya kucheza michuano hiyo.

Katika hatua nyingine, Rage alisema leo wanasaini mkataba mpya na TBL ambapo wameshakubaliana na kampuni hiyo kuwaongezea fedha za mshahara kutoka sh. milioni 16 mpaka sh. milioni 26 na pia kuwapa basi kubwa la kisasa la Marcopolo, kutoka Brazil.

Alisema pia kampuni hiyo imekubali kutoa sh. milioni 20 kila wanapofanya Mkutano Mkuu, kwa ajili ya kufanikisha shughuli mbalimbali za mkutano huo.

2 comments:

  1. Ndugu Mwandishi Experance sio timu ya Misri ni ya Tunisia. na pia Simba haitocheza na Esperance itacheza na Wydad Casablanca ya Morocco. tuache kupotosha watu. na kabla ya kutuma habari inabidi muihakiki.
    mdau wa majira UK.

    ReplyDelete
  2. Bwana, mkono wakati mwengine hufanya makosa
    kama alivo binaadamu kwahivo hakuna haja ya kutuhumiana kwa upotovu.

    ReplyDelete